Suleiman Msuya
WACHUMI wamesema mfumuko wa bei ya
vyakula unaolikumba Taifa na nchi nyingine za Afrika Mashariki ni wa mpito na
ulisababishwa na ukame ulitokea siku za nyuma. Lakini wakaishauri Serikali
ichukue hatua. Aidha, wabunge wamemwomba Spika wa Bunge, Job Ndugai kutoa
nafasi kwao kujadili hali hiyo waliyosema ni mbaya.
Wakizungumza jana katika mahojiano na
JAMBO LEO, wataalamu hao walisema hakuna sababu ya kufikiria sana jambo hilo
wakieleza linaweza kupata ufumbuzi Taifa likiweka mikakati sahihi na kutumia
mvua zinazonyesha kwa usahihi.
Mbunge wa Jimbo la Mchinga CUF, Hamidu
Bobali alisema Serikali inapaswa
kuruhusu mahindi yaliyo kwenye maghala ya wakala wa hifadhi ya chakula
ya Taifa yaingizwe katika soko ili kuwawezesha wananchi kupata chakula kwa bei
sawa.
“Pia, tunaomba Spika Job Ndugai atoe
nafasi kwa wabunge kujadili hali kwani hali halisi ni mbaya na mimi katika
jimbo langu nimeona hali mbaya nadhani kila mbunge atatoa ya moyoni,” alisema
Bobali.
Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula
alisema wanasubiri bajeti ya Wizara Kilimo Mifugo na Uvuvi ili waone mipango
yao ndiPo watajua nini cha kufanya.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha
Mzumbe (MU), Profesa Damian Gabagambi alisema kinachoonekana kwa sasa ni tukio
la mpito ambalo litatulika baada ya muda mfupi hasa ukizingatia mvua zimeanza
kunyesha.
Alisema mvua zinazonyesha zitasaidia
kupatika kwa chakula hivyo mfumo huo wa bei za vyakula utadhibitika kwa haraka
hivyo wananchi kuhimili gharama za manunuzi.
“Mimi naliona kama suala la mpito kwa
sababu vyakula vingi tunavyokula vinatoka shamba moja kwa moja tofauti na
wenzetu ambao wanatumia vilivyopo madukani, hivyo mvua zinazonyesha zitatatua
tatizo, ila inapotokea kuna kitu kinaingilia uzalishaji wa mazao ni lazima
mfumo uongezeke na ukame ni sababu,” alisema.
Alisema chanagmoto ambayo iliikuta
Tanzania iligusa katika Ukanda wate wa Afrika Mashariki hivyo ni lazima athari
zionekanekane kwa haraka.
Profesa Gabagambi alisema kinachotakiwa
ni wizara ya kilimo kupitia kitengo cha usalama wa chakula kujua hali hali ya
chakula ili waweze kushauri Serikali kabla hali hiyo haijafikia.
Alisema iwapo kutakuwa na ushirikiano
baina ya kitendo hicho na wazalishaji inaweza kuwa njia sahihi ya kutambua
upungufu wa chakula na nini kifanyike wakati huo.
Aidha, alisema suala hilo haliwezi
kuchukuliwa kisiasa kwani ni dhahiri sababu za msingi zipo kwa hali hiyo
kuwepo.
Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi wa
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk. Christopher Awinia alisema sababu ya
mfumo wa bei ya vyakula unachangiwa msimu wa kilimo hali ambayo wakulima wengi
wanazalisha.
Alisema sababu nyingine inahusu mgogoro
ya kivita katika nchi za Burundi na Sudani Kusini hali ambayo inaongeza hitaji
la chakula kutokana na kundi hilo kutojihusisha na kilimo.
“Pia miundombinu kuharibika inaweza kuwa
sababu ya kukosekana kwa vyakula hasa kipindi hiki cha mvua na pindi
kikipatikana bei inakuwa kubwa,” alisema.
Aidha, alisema sera ya kuagiza vitu
kutoka nje inaweza kuwa imeaathiri kutokana na kodi ambazo zinakatisha tamaa
kwa wafanyabiashara.
Mhadhiri mwandamizi huyo alisema njia ya
kusaidia katika maeneo ambayo mfumuko umezidi kuwa mkubwa ni vema Serikali
kugawa chakula na kuweka mazingira mazuri ya kuagiza kutoka nje.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu,
mfumuko wa bei wa Taifa kwa kipimo cha mwaka umebaki kuwa asilimia 6.4 kama
ilivyokuwa mwaka uliopita, lakini fahirisi za bei zimeongezeka hadi Sh.109.4
Aprili 2017 kutoka Sh.102 Aprili 2016.
"Mfumuko wa bei kwa kipimo cha
mwaka umebaki kuwa asilimia 6.4 kama ilivyokuwa Machi 2017, kasi ya upandaji wa
bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioisha Aprili imekuwa sawa na Machi
2017,"alisema
Pia alisema mfumuko wa bei wa bidhaa za
vyakula na vinywaji baridi kwa Aprili 2017 umeongezeka hadi 11.8 kutoka
asilimia 11.0 ilivyokuwa Machi.
Aidha mfumuko wa bei kwa kipimo cha
mwaka kwa bidhaa za vyakula nyumbani na migahawani Aprili 2017 umeongezeka hadi
asilimia 12.0 kutoka asilimia 11.7 kwa Machi 2017.
Alisema badiliko la fahirisi za bei kwa
bidhaa sisizo za vyakula umepungua kidogo hadi asilimia 3.4 Aprili kutoka
asilimia 3.6 kwa Machi.
Akizungumzia kuhusu ukuaji wa dhamani ya
shilingi, Kwesigabo alisema uwezo wa shilingi ya Tanzania katika kununua
bidhaa na huduma umefikia Sh.91.71, Aprili 2017 ikilinganishwa na Sh. 92. 21
ilivyokuwa Machi 2017.
0 comments:
Post a Comment