Mery Kitosio, Meru
KANISA la KKKT, Dayosisi ya Meru imejiwekea utaratibu wa
kutumia Sh. milioni 40 kwa mwaka kwa ajili ya kuwasomesha wanafunzi wanaotokea
familia zisizo na uwezo pamoja na watoto wa kike wanaotokea kabila la Kimasai
ambao wanaozeshwa kwa nguvu.
Hayo yalisemwa na Askofu Mkuu wa Dayosisi hiyo Elias
Kitoi alipokuwa akizungumza katika sherehe za mahafali ya sita ya kidato cha
sita ya Seminari ya Ailanga.
Askofu Kitoi alisema kuwa wamekuwa wakitafuta wale watoto
wa masikini ambao wanatokea shule zote zilizopo ndani ya eneo la meru na
hata watoto wa kike ambao mara nyingi wamekuwa wakikosa elimu kwa ajili ya
kuozeshwa kwa nguvu kwa kuwasomesha hadi kilele wanachopenda ili kuwawezesha
kutimiza malengo ya elimu kama zilivyo jamii nyingine.
"Tulishawasaidia wanafunzi wengi sana kwa utaratibu
huu kwani sisi tunaangalia tu wale wanafunzi ambao wanafanya vizuri katika
mitihani ya mwisho ya kidato cha nne na sita na kuamua kuwaendeleza hadi
chuo kikuu kwa kuwafadhili sisi pamoja na wafadhili kutoka nchi za nje ambao
nao waliupenda sana huu utaratibu wetu,"aliongeza Askofu Kitoi.
Alisema mbali na kuwasaidia watoto hao wamekuwa pia
wakitoa kipaumbele sana sehemu ambazo hadi sasa elimu haithaminiwi kama sehemu
za umasaini ambapo kumeoneka kuwa elimu kwa watotot wa kike haipewi kipaumbele
na hivyo kufanya maeneo hayo kubaki nyuma kimaendeleo.
Awali, mkuu wa seminari hiyo Wilium Lowasa aliiomba Serikali
kutupia jicho la pili upatikanaji wa maji safi na salama shuleni hapo kwani
yaliyopo kwa sasa yana kiwango kikubwa cha floride hivyo kuufanya shule kutumia
gharama kubwa mno kwa ajili ya utafutaji wa maji safi kwa usafiri wa gari.
Aidha alidai kuwa kwa sasa shule hiyo imejiwekea mikakati
ya kuhakiisha inakuwa ya kwanzz kitaifa kwa kubadilisha mfumo wa mitihani
ambapo kwa sasa wamekuwa wakitunga mitihani iliyo sawa na kitaifa ili
kuwajengea wanafunzi uwezo wa kupambana na mitihani yao ya mwisho.
0 comments:
Post a Comment