Grace Gurisha
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam
inatarajia kusikiliza kesi ya madai iliyofunguliwa na wanafunzi 316
waliofukuzwa katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph kwa madai ya kutokuwa na
sifa za kudahiliwa kwenye vyuo vikuu nchini, wakidai fidia ya Sh. bilioni sita,
Juni 29 mwaka huu.
Kesi hiyo itasikilizwa mbele ya Jaji Wilfred Ndyansobera,
baada ya pande zote kushindwa kumaliza kesi hiyo nje ya Mahakama. Wanafunzi hao
wamefungua kesi hiyo dhidi ya chuo hicho na Bodi ya Mikopo na Tume ya Vyuo
Vikuu (TCU).
Wanafunzi hao walifungua kesi hiyo namba 122 mahakamani
hapo kupitia wakili wao Emmanuele Muga. Wanafunzi hao wanadai Sh.bilioni moja
kwa ajili ya mjumuisho wa ada na vifaa tangu wakae chuoni hapo, huku Sh.bilioni
tano kama fidia.
Katika madai hayo walieleza kuwa TCU iliwaruhusu kudahili
wanafunzi wa Shahada ya Sayansi kwa miaka mitano, huku miaka miwili ikiwa kwa
ajili ya kusafisha cheti cha kidato cha nne na miaka mitatu iliyobaki kwa ajili
ya kusomea Shahada.
Wamedai kuwa baada ya TCU kutoa tamko Mei mwaka jana kwamba wanafunzi hao hawana sifa walirudi
nyumbani, huku miongoni mwao wakiwa tayari wamesoma kwa miaka mitatu, miwili na
mmoja.
Wanafunzi hao wamedai kuwa awali wakiingia chuoni hapo
walilipa karo iliyojumuhisha na vifaa vya chuo kwa Sh.milioni moja kwa kila
mwanafunzi. Awali mahakama hiyo ilikubali kutoa kibali cha kufungau kesi ya
uwakilishi kwa wanafunzi 316, ambao watawakilishwa na Ramadhan Kipenya, Innocent Peter, Oswald
Mwinuka na Feith Kyando.
Hivyo kutokana na kufukuzwa chuoni hapo, wameiomba
mahakama iiamuru TCU na chuo cha Mtakatifu Joseph kuwalipa kiasi hicho cha
Sh.bilioni moja kwa ajili ya wanafunzi wote na Sh.bilioni tano kama fidia.
0 comments:
Post a Comment