…Wapongeza utumbuaji, wakosoa mikataba ya madini


Sharifa Marira na Suleiman Msuya


Profesa Sospeter Muhongo
SAA chache baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, na kuwachukulia hatua watendaji wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), wabunge na wanasiasa wamepongeza uamuzi huo na kuanika uozo katika mikataba ya madini.

Wakati maoni hayo yakitolewa, Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ya mwaka 2017/18 iliyokuwa isomwe leo Dodoma, imesogezwa mbele hadi Jumatatu huku kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia ikieleza kushangazwa na ripoti ya uchunguzi wa makinikia na kuahidi kutoa ufafanuzi baada ya kuipitia kwa kina.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika (Kibamba) alisema hatua zilizochukuliwa hazitoshi kwa maelezo kuwa mzizi wa tatizo hilo ni Sheria ya Madini ya Mwaka 2010.

“Mikataba mibovu iliyoingiwa ndiyo imeweka vifungu vya mchanga kusafirishwa nje, vinatoa umiliki mdogo wa Serikali. Mikataba hiyo inaonesha kuwa yaliyo kwenye mchanga ni mali ya mwekezaji,” alisema Mnyika.

“Tulitarajia leo Rais aseme ukweli kama haya yote alikuwa anayajua na si mapya, maana tulishayazungumza sana na yeye alikuwa Waziri anayajua yote. Mikataba inapaswa kuvunjwa na sheria ya madini kuletwa bungeni irekebishwe,” alisema Mnyika.

Alisema Rais Magufuli alipaswa kuwataja mawaziri wote walioingia mikataba mibovu, huku akimtaja Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ambaye alipata kuwa Waziri wa Nishati na Madini mwaka 1994.

Huku akikosoa kauli ya Rais kuwa dhahabu zilizogundulika ni mali ya Serikali, Mnyika alisema licha ya kuwa dhahabu hizo ni mali ya mwekezaji kwa mujibu wa mkataba na kwamba uamuzi huo utaliingizia Taifa hasara.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Dotto Biteko aliupongeza uamuzi huo na kubainisha kuwa Rais ameyafanyia kazi maoni ya Kamati hiyo ipasavyo.

Biteko ambaye pia ni Mbunge wa Bukombe alisema Taifa lilikuwa linaibiwa mabilioni ya fedha kwa maelezo kuwa kuna madini yaliyokuwa hayalipiwi mrabaha.

Alipoulizwa sababu za Kamati kushindwa kubaini wizi huo, alisema: “Katika vikao vya Kamati, Wizara ilikuwa ikiwasilisha taarifa za uongo tofauti na hali halisi kwenye Wizara ila Kamati iliyoundwa na Rais imethibisha kila kitu.”

Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema: “Hii si hadithi mpya, kwamba tunaibiwa kwenye madini, mimi niliiandika mwaka 2008 nikaeleza namna kampuni za madini zinavyoficha mapato stahiki kukatwa kodi.”

Lissu ambaye alieleza kwa kirefu alivyoanza harakati za kueleza nchi inavyoibiwa madini tangu mwaka 2002, alisema tume nyingi zilizoundwa kuchunguza sekta ya madini zilieleza jinsi Taifa linavyoibiwa.

Alisema tatizo lilianza mwaka 1998 baada ya Bunge kutunga na kupitisha kwa dharura sheria alizoziita za hovyo, ambazo ni Sheria ya Kodi, Sheria ya kufanya marekebisho mbalimbali katika sheria ya fedha na Sheria ya uwekezaji ya Taifa.

“Hizi ndizo tatizo kwa nchi. Mwaka 1998 ikatungwa sheria ya madini iliyorekebishwa mwaka 2010 baada ya maoni ya Tume ya Bomani. Sheria hii ilisema madini yanayochimbwa ni mali ya mwekezaji kwa mujibu wa sheria za Tanzania,” alisema Lissu.

“Sheria hii inasema sehemu ya madini watakayoshindwa kusafishia hapa watayapeleka nje. Katika mchanga kuna madini ya shaba, fedha na dhahabu kidogo. Mkataba unasema hayo madini mengine matatu wala hawayatozi kodi.”

Lissu alisema mbali na Profesa Muhongo, hata Naibu Waziri, Dk Medard Kalemani naye anapaswa kuchukuliwa hatua, kwa maelezo kuwa amekuwa mwanasheria wa wizara hiyo kwa muda mrefu.

“Kwa nini anamfuata Kafumu (Dalali), kwa sababu alikuwa Kamishna wa Madini, Mikataba ya Madini ilianza kuingiwa wakati kamishna akiwa Grey Mwakalukwa, aanze na huyu,” alisisitiza.

Mwanasheria Mkuu huyo wa Chadema alisema wawekezaji wa madini wanalindwa na mikataba waliyoingia na Serikali na kwamba Tanzania ni nchi mwanachama wa Multilateral Investment Guarantee Agency (MIGA).

“Ukiwa mwanachama, wawekezaji wakileta mali zao kwako ukachukua mali zao kama alivyofanya Rais utashughulikiwa huko kwenye mahakama za kimataifa,” alisema.

“Rais wetu kama kawaida yake ameshauriwa? Amejiingiza kwenye mgogoro mkubwa, anafikiri anapata sifa ndogondogo hapa. Haya mambo tumeyapigia kelele kwa miaka mingi.”

Alimtaka Rais Magufuli kuiondoa Tanzania kwenye MIGA ili wawekezaji wasiweze kushitaki kokote.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk George Kahangwa alisema ni wakati mwafaka kwa Watanzania kuungana na Rais.

Alisema ni wakati mwafaka kwa pamoja kusema wizi sasa basi na kuhakikisha wahusika wote wanachukuliwa hatua wawe wazawa au wageni.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo