Mwandishi Wetu, Simiyu
SIKU chache
baada ya Serikali kuweka hadharani majina ya watumishi wa umma wenye vyeti bandia,
baadhi wameanza kukimbia madeni waliyokopa kwa watu binafsi, huku wategemezi
wao wakikosa mahali pa kukimbilia.
Uchunguzi
uliofanywa mkoani hapa umebaini kuwa baadhi ya watumishi wa umma hasa walimu
waliokuwa wamekopa kwa watu binafsi, wameanza kukimbilia kusikojulikana, huku baadhi
yao wakizima simu na kuhama makazi yao kimyakimya.
Mmoja wa
wafanyabiashara wa Bariadi, Mashaka Magembe alisema amekuwa akikopesha walimu
kwa riba, lakini baada ya kubaini kuwa baadhi yao wameondolewa kwenye utumishi
wa umma kwa kuwa na vyeti bandia alianza kuwatafuta ili kulipwa madeni, lakini
hakufanikiwa.
“Baada ya kuona
majina yao kwenye orodha, niliwapigia simu lakini hawakunipa ushirikiano kama
awali…mmoja nilikuwa namdai Sh 300,000, nilipompigia simu alisema tukutane
mtaani badala ya nyumbani kwake na nilipofuatilia kwake nikakuta ameshahama,”
alisema Magembe.
Aliongeza kuwa
baadhi yao walirejesha fedha kidogo huku wakisema kuwa hali ni mbaya kulingana
na majina yao kuwa kwenye orodha ya watumishi walioghushi vyeti huku wakiomba
awasimamishie riba na watakuwa wanalipa kidogo kidogo.
Alisema hadi
sasa hajui aliko mmoja wa wadeni wake wala simu yake haipatikani na ameshahama
alikokuwa akiishi wakati kwenye mkataba wa mkopo aliweka dhamana ya seti ya
sofa, televisheni, friji na kitanda.
Joel Peter
ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Ualimu Tabora, alisema hatamalizia masomo yake
kutokana na wategemezi wake wote kubainika kuwa na vyeti bandia.
Alisema kaka yake ambaye ni mwalimu wilayani Itilima amebainika kuwa na vyeti bandia, hivyo ana wasiwasi juu ya upatikanaji wa fedha za kumalizia masomo yake ya ualimu.
“Kaka na mkewe
wote wamebainika kuwa na vyeti bandia na ndio walikuwa wakinisomesha, sasa
sijui itakuwaje na wazazi wangu walishafariki dunia,” alisema Joel huku
akiiomba Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia wanafunzi walio masomoni.
Habari zaidi
zilieleza kuwa baada ya agizo la Rais John Magufuli kutaka watumishi wenye
vyeti bandia kutoweka ofisini, baadhi ya maofisa utumishi mkoani hapa wameanza
kutoa barua za kuwafukuza kazi watumishi hao mara moja.
0 comments:
Post a Comment