Grace Gurisha
Tundu Lissu |
MALUMBANO makali yaliyotawaliwa na kejeli yameibuka kati
ya mawakili wanne wakiongozwa na Tundu Lissu dhidi ya Wakili wa Serikali, Salum
Mohamed, kwenye kesi ya tuhuma za kuzuia Jeshi la Polisi kufanya kazi yake,
inayomkabili muasisi wa mtandao wa Jamii Forums, Maxence Melo.
Malumbano hayo yaliibuka juzi wakati Meneja wa Usajili wa
Kikoa cha Tanzania cha co.tz kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),
Habibu Rashid akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Mara kwa mara Hakimu huyo aliwakatisha mawakili hao,
kutokana na kurushiana vijembe kwa lengo la kumchanganya shahidi na Wakili
Mohamed.
“Wewe Mohamed kuwa makini na kazi yao, fanya kazi hawa
wako wengi wanataka tu kukuchanganya, wewe endelea kumwongoza shahidi wako,” alisema
Hakimu Nongwa.
Wakati Mohamed anamwongoza Rashid kutoa ushahidi wake,
mara nyingi mawakili wa Melo walisimama kumlalamikia Hakimu, kuwa wakili huyo anampa
majibu shahidi wake kutoka na anavyomwuliza maswali.
Hali hiyo ilisababisha Mohamed kukasirika kwa kuona kuwa
mawakili hao wanamwingilia kazi yake, ndipo maneno ya kejeli yalipokuwa
yakitoka kuwa wakae kimya na kushangaa wanachoogopa au pengine hawakuwa wamejiandaa
huku wakinyoosheana vidole.
Malumbano hayo yalichukua sura mpya, baada ya wakili
mwingine wa Serikali ambaye alikuwa anasikiliza kesi hiyo, Baltrida Mushi kumgeukia
wakili mwingine wa Melo, Peter Kibatala na kumnyooshea kidole akimtaka amwache
Mohamed amalize kuongea.
Kitendo hicho kilimkasirisha Kibatala na kumfuata Mushi
alipokaa huku akimfokea kuwa yeye nani katika kesi hiyo hadi amnyamazishe
kuzungumza wakati ni haki yake, akamwomba Hakimu amshughulikie kwa sababu hana
nidhamu.
“Halafu huyu hausiki kabisa katika kesi hii, sijui nini
kimemtuma kufanya hivyo, lakini keshajionya mwenyewe, tuendelee,” alisema
Hakimu Nongwa.
Pia jambo lingine ambalo liligeuka kituko ndani ya chumba
cha Mahakama ni shahidi Rashid alipokubali kutoa waraka aliopewa na Kibatala
kama kielelezo katika kesi hiyo, huku akieleza kuwa uko sahihi na haoni kama una
tatizo lolote.
Muda huo mawakili wa Serikali waliokuwa ndani ya chumba
hicho akiwamo Mohamed, walijitahidi kumwonesha kwa ishara shahidi huyo akatae,
lakini yeye aliendelea kuwasisitiza kuwa uko sahihi.
Waraka huo ulionesha kuwa Jamii Forums imesajiliwa na
inaonesha ni lini itamaliza muda wake, wakati mahakamani hapo Melo anashitakiwa
kuwa hakusajili mtandao huo, ambapo Mohamed alijitahidi kuiomba Mahakama
isipokee waraka huo kwa madai kuwa haukuwa halisi. Uamuzi wa hoja hizo
utatolewa Juni 5.
Melo anatuhumiwa kuwa siku zisizofahamika kati ya Mei 10
na Desemba 13 mwaka jana, akiwa ofisini kwake alizuia upelelezi kufanywa na Jeshi
hilo kwa kushindwa kukubaliana na amri za kutoa taarifa alizokuwanazo kwenye
mtandao wake.
0 comments:
Post a Comment