Dalila Sharif
SHEKHE Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salim, amewaomba wafanyabiashara wasipandishe
bei ya bidhaa katika kipindi cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Alitoa maombi
hayo jana kutokana na alichosema ni tabia ya baadhi ya wafanyabiashara
kupandisha bei ya bidhaa zao wakati wa Mfungo huo ili kujinufaisha binafsi.
“Vyakula
vinapanda katika kipindi cha Mfungo na kuwasababishia baadhi ya wafungaji kutomudu
hali hiyo, vitu vinakuwa na bei kubwa kuliko miezi ya kawaida,” alisema Salim.
Alisema
ni vema Waislamu kujianda katika kipindi cha kuikaribisha Ramadhan kwa kutenda
yaliyo mema na kuacha mabaya yasiyompendeza Mungu.
“Mwezi
Mtukufu wa Ramadhan ni wa kila Mwislamu, kila mmoja anatakiwa kutii kwa kufunga
na wala si jambo la hiyari ni lazima, kwa kila mwumini mwenye uwezo na vigezo
vya kufunga,” alisema Alhad.
Aliwataka
Waislamu kuwasaidia wasiojiweza kama kukaa na yatima na kuwalisha vyakula akisema
hali hiyo itawajengea misingi bora katika kumsaidia asiye na kitu.
Katika
hatua nyingine, aliwataka Waislamu kuliombea amani Taifa na watu wa mkoa wa
Pwani waliokabiliwa na matukio ya mauaji ya kutumia silaha akisema:
“Nawaomba
Waislamu tuiombee nchi yetu ya Tanzania amani hasa wenzetu wa mkoa wa Pwani kwa
majanga yaliyotokea na tuombee vyombo vyetu vya ulinzi kuimarika ili kulinda na
kudumisha amani ya nchi yetu.”
0 comments:
Post a Comment