Mwandishi Wetu
ABIRIA wa treni ya Reli ya Kati kutoka Bara kwenda Dar es
Salaam wamesota kwa saa nane Morogoro wakihamishia
mizigo kwenye mabasi baada ya daraja la Mazimbu kusombwa na maji kutokana na
mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo.
Abiria hao zaidi ya 500 waliotoka Kigoma Jumatatu saa 6
mchana, walishuka kwenye treni hiyo eneo la Lukobe usiku wa kuamkia jana
na kupakua mizigo kwenye treni hiyo na kuipakia kwenye mabasi na kwenda
Morogoro Mjini ili kupanda treni nyingine ya kwenda Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa abiria waliozungumza na gazeti hili jana,
walitumia saa nane kuhamisha mizigo na kutoka eneo hilo hadi stesheni ya
Morogoro huku wakinyeshewa mvua.
"Tulifika Lukobe saa nne usiku na kuhamisha mizigo
kutoka kwenye treni. Binafsi nilikuwa na mizigo mingi na watoto wawili. Huku
nanyeshewa mvua, nililazimika kukubaliana na hali halisi," alisema mmoja
wa abiria hao, Jackline Jacob.
Treni hiyo iliwasili Dar es Salaam jana saa 5.15 asubuhi
badala ya Jumanne asubuhi, kutokana na ajali mbili za treni, ikiwamo
iliyotokea Lukobe na kusababisha abiria kuhamishiwa
kwenye mabasi.
"Kuna mizigo nimeibiwa kutokana na wingi wa watu na
kutokuwa na ulinzi. Pia tulihanishwa usiku, kwa hiyo ulikuwa ni usumbufu wa
hali ya juu. Kutoka tulikoteremkia hadi Morogoro Mjini pia ni mbali,"
alisema Josephine Cleophas wa Dar es Salaam.
Msemaji wa TRL, Midraj Maez akizungumzia tukio hilo,
alisema hali hiyo ilitokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani
Morogoro na maeneo mengine nchini.
“Tulishazungumzia hilo pale Morogoro, lakini kifupi mvua
ndiyo sababu ya tatizo hilo, lakini linafanyiwa kazi kurekebisha,” alisema.
0 comments:
Post a Comment