Fidelis Butahe
Angela Kairuki |
WAKATI watumishi 9,932 wakiondolewa kwenye
ajira serikalini baada ya kubainika kuwa na vyeti bandia, wanasheria wamesema ingawa
watu hao wamefanya kosa, ubinadamu ulipaswa kuzingatiwa kuwaondoa.
Pia wametaja mambo matatu ya kuwanusuru
wakisema: “Tutumie sheria kuwaondoa. Lakini sheria wakati mwingine si kama
chuma.”
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati
tofauti, walitaja mambo hayo kuwa ni kuachishwa kazi kwa maslahi ya Taifa na
kulipwa mafao yao, kusimamishwa kazi kwa miaka miwili na kutakiwa kurudia
mtihani wa kidato cha nne ili kupata cheti na kuchukuliwa hatua kulingana na
ukubwa wa makosa yao.
Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Kitivo cha Sheria, Dk Onesmo Kyauke
alisema: “Kwa maana ya sheria hata kama ulikuwa profesa lakini
ukabainika umeghushi cheti, elimu yako inapoteza maana. Yaani unakuwa kama ghorofa lililobomolewa
upande mmoja.
“Wenye vyeti bandia lazima waondolewe lakini
zaidi ya sheria kuna ubinadamu pia. Lazima tukubali kuwa mfumo wa ukaguzi
haukuwa mzuri. Pia miaka ya nyuma kupata elimu ya sekondari ilikuwa ngumu sana,
wapo waliotumia njia za mkato,” alisema.
Tangu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora itoe ripoti ya uhakiki iliyobaini idadi hiyo, hali
imekuwa mbaya katika ofisi za umma kutokana na watumishi wengi kulazimika
kuachia ngazi, huku baadhi ya ofisi huduma zikizorota kutokana na waliotajwa
kuamua kutokwenda ofisini.
Miongoni mwa watumishi hao wapo ambao
walitajwa kwenye orodha hiyo licha ya kuwa na vyeti, jambo ambalo Mwanasheria
Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliliambia gazeti hili kuwa ikibainika ni kweli,
watumishi hao ni lazima warejeshwe kazini na kusafishwa tuhuma dhidi yao.
Akipokea ripoti hiyo, Rais John Magufuli
aliagiza waliotajwa kuondoka kazini mara moja na watakaobaki hadi Mei 15,
wafikishwe mahakamani.
Kwa hali hiyo, juzi Katibu Mkuu Ofisi ya
Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro
alizitaka mamlaka zilizoathirika kuomba vibali vya dharura vya ajira, huku
akitangaza Serikali kuajiri watu 15,000 kati ya sasa na Juni 30.
Katika ufafanuzi wake, Dk Kyauke
alisema: “Kama Taifa lazima tukubali kuwa kosa limeshafanyika sasa tunafanyaje?
Nadhani Serikali ingetazama waliofanya kosa hilo ndani ya miaka 10 iliyopita wakaondolewa.
Waliobakiza miaka 10 kustaafu wangeachwa. Tutafute namna ya kibinadamu tu.”
Akitolea mfano wa walimu wa shule za
msingi, alisema mshahara wao ni mdogo na wapo waliobakiza miaka miwili
kustaafu.
“Hawa maana yake hawapati mafao yoyote.
Huku ni kuwasababishia kifo tu. Tutumie
sheria kuwaondoa, lakini sheria wakati mwingine si kama chuma, unaweza kusaka
suluhu kwa njia nyingine,” aliongeza.
Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Dk
James Jesse alisema: “Hawa watu walikaa kazini muda mrefu na miaka ya nyuma
hatukuwa na mfumo wa kukagua na kujua kama vyeti ni bandia au la.”
Aliongeza: “Nadhani kulihitajika aina
fulani ya ubinadamu. Unajua katika kughushi kuna tofauti, wapo waliochukua
vyeti vya wengine, wapo waliofuta majina na kuweka yao. Katika uchambuzi
wangechukuliwa hatua kulingana na makosa yao.”
Alisema watu waliotumia vyeti vya kidato
cha nne vya watu wengine na kuendelea na masomo walipaswa kuangaliwa kwa jicho
la pili.
“Inaweza kuwa ngumu kufanya uchambuzi,
ila wenye kesi ndogo ubinadamu ulipaswa kuzingatiwa. Wapo wanaohitaji msamaha,”
alisema.
Julius Mtatiro alisema: “Wenye vyeti bandia
hawakupaswa kufukuzwa. Kwanza, ilitakiwa kuangalia miongoni mwao je wapo
walioonesha weledi kazini? Nasema hivi kwa sababu wapo wenye vyeti bandia
lakini wana shahada na ni watendaji wazuri.
“Pia wapo madaktari bingwa wenye vyeti bandia
vya kidato cha nne, lakini kwa sasa wanaaminika sana, sasa huyu unamfanyaje.
Unamfukuzaje huyu?” Alihoji.
Alisema baadhi ya watumishi walipaswa
kuandaliwa programu maalumu ili kurudia kidato cha nne na kupata cheti halali au
kuachishwa kazi kwa maslahi ya umma, ikiwa ni pamoja na kulipwa mafao yao yote.
“Wapo walioitumikia Serikali kwa miaka
30, mtu huyu unamfukuzaje hivi hivi? Si bora wapewe likizo ya miaka miwili na
kulipwa nusu mshahara ili wakasome na kupata vyeti vya kidato cha nne,”
alisema.
Akizungumzia iwapo itabainika baadhi yao
wana vyeti halali, Lissu alisema: “Ikibainika, watatakiwa kurejeshwa kazini na
kusafishwa kwa kuchafuliwa.
“Kama mtu ana vyeti halali halafu
anatangazwa dunia nzima, ana vyeti bandia, jambo ambalo sheria inasema ni kosa
la jinai la kifungo na adhabu yake ni kifungo cha miaka saba gerezani.
Ikithibitika wamesingiziwa, sheria ipo wazi wala hawahitaji kulalamika kuwa
wameumizwa,” alisema.
Alisema ikiwa watumishi hao wana vyeti bandia
nao wanapaswa kusikilizwa, kusisitiza kuwa suala lao la vyeti bandia lilitolewa
na upande mmoja tu wa Serikali.
“Wanahukumiwa wamefanya makosa, ni
wahalifu na wameiibia Serikali, je ni halali? Wanaweza kwenda mahakama za kazi
na kudai kufukuzwa kazi kwa utaratibu usio wa kisheria, ikithibitika wanatakiwa
kurudishwa kazini na kulipwa mafao yao,” alisema Lissu.
Alisema utaratibu wa kisheria wa
kumfukuza kazi mtumishi wa umma ulipaswa kufuatwa, ikiwa ni pamoja na
kufunguliwa mashitaka ya kinidhamu ya kufukuzwa kazi.
“Tunafanya mambo utadhani hakuna sheria.
Mfano Serikali tangu mwaka 2012 ilitoa vigezo vyake vya waomba ajira kwa wakuu
wa mikoa na wakuu wa wilaya, lakini leo hii hawajaguswa wakati sheria iliwekwa
na Serikali,” alisema.
Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha
Wanasheria wa Tanganyika (TLS) alihoji sababu za uhakiki huo wa vyeti kutokugusa
vyombo vya ulinzi na usalama nchini.
“Iweje Jeshi lisiguswe, Magereza na
Polisi, ina maana huko wako safi?” Alihoji.
0 comments:
Post a Comment