Grace Gurisha
Khamis Mgeja |
MWENYEKITI wa Wakfu wa Tanzania Mzalendo, Khamis Mgeja,
ameishauri Serikali kuwa sikivu, akiitaka kufanya hivyo ikikumbuka kuwa ni mali
ya umma na si kampuni binafsi.
Akizungumza na JAMBOLEO jana kwa njia ya simu, Mgeja
alisema wakati Serikali ikiingia madarakani ilikuwa na misingi mizuri, lakini sasa
imebomoka kwa kasi kubwa kwa sababu si sikivu.
“Hili suala halina afya katika jamii, kwa hiyo Serikali
inatakiwa iwe sikivu kwa sababu ni mali ya umma, lakini kinachofanywa ni
kuhangaika na watu wachache, badala ya kusimamia misingi ya Katiba,” alisema
Mgeja.
Alisema hali hiyo imesababisha nchi kugubikwa hofu na
wananchi kupandikizwa chuki ikitokana na watu kuzibwa midomo ya kuongea, na
hivyo Serikali kukosa cha kufanya kutokana kwa kukosa kupata mawazo.
Alibanisha kuwa raia wanaendelea kufuga nyongo jambo
ambalo si zuri katika nchi kama Tanzania ambayo ndiyo inatafuta maendeleo kwa
hali na mali.
“Ombi langu kwa Rais Magufuli (John) aheshimu misingi ya Katiba,
kwa sababu siku anaapishwa, aliapa kuilinda, iweje sasa aende kinyume na kiapo?
Demokrasia katika nchi zote duniani ni kipimo namba moja cha misingi ya
maendeleo.
“Kama hakuna demokrasia ya kweli, huru na uwazi haya
mambo ya ndege, sijui treni ni kazi bure, kwa sababu hayatakuwa na thamani kama
watu hawana uhuru wa kutosha. Na suala hili limesababisha Taifa kupata hasara
kubwa, wafadhili wamesitisha pia misaada,” alisema.
Akizungumzia watu kutishiwa bunduki hadharani, alisema si
jambo la haki, kwa sababu mikono ya Dola inawaonesha raia waziwazi mambo yasiyo
salama kwao, kwa sababu itafika siku watazoea milio ya risasi.
Alisema wakishaizoea, siku askari Polisi akitoa chombo
chake cha moto, raia wataokota mawe na kuwapiga na bila kujua wataanza kuona
kama wananchi ni wakaidi, huku wakisahau kuwa wao ndio visababishi vya yote
hayo.
0 comments:
Post a Comment