Sharifa Marira, Dodoma
ZAIDI ya watu
7,000 wamekamatwa kwa tuhuma za ujangili katika mwaka 2016/17 kutokana na doria
iliyofanyika kwa siku 349,103.
Waziri wa
Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alibainisha hayo bungeni jana
alipowasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Wizara yake kwa
Mwaka wa Fedha 2017/18, ambapo alieleza lengo la kuweka doria kuwa ilitokana na
matukio ya ujangili na biashara ya haramu ya wanyamapori.
Alisema Idara ya
Wanyamapori, TANAPA, NCAA na TAWA, waliendesha doria ndani na nje ya hifadhi
hatua iliyofanikisha kukamata watuhumiwa 7,085.
Alisema katika
operesheni hiyo, meno ya tembo 129 na vipande 95 vyenye uzito wa kilo 810.03
vilikamatwa sambamba na silaha za kivita 48, silaha za kiraia 150, risasi
1,058, magobori 406, silaha za jadi 22, 307 na roda 120,537.
Profesa Maghembe
alitaja vingine vilivyokamatwa kuwa ni pikipiki 189, baiskeli 214, magari 20,
ng'ombe 79,831 na samaki kilo 4,043 ambapo kesi 2,097 zilifunguliwa kwenye
mahakama mbalimbali na 802 kumalizika huku kesi 262 zenye watuhumiwa 472 zikimalizika
kwa wahusika kufungwa jela jumla ya miezi 42,153 na kesi 43 zilizokuwa na
watuhumiwa 79 wahusika kuachwa huru.
Alisema kesi 276
zilimalizika kwa watuhumiwa 469 kulipa faini ya jumla ya Sh milioni 452.1 na
kesi 966 ziliendelea katika mahakama mbalimbali nchini.
Alieleza kuwa katika
kuhakikisha Wizara hiyo inadhibiti ujangili na
biashara haramu
ya nyara za Serikali, ilianzisha kikosikazi maalumu, kutumia teknolojia ya
ndege zisizo na rubani na mbwa maalumu wa kunusa.
Alisema mwaka
2016/17, doria maalumu za kiintelijensia zilifanyika
kwenye kanda
zote za kiikolojia na kubaini wahalifu 906 wa
ujangili ambapo
384 walikamatwa na kufikishwa mahakamani.
Profesa Maghembe
alisema taarifa za kiintelijensia zilionesha kuwa
majangili
wakubwa wanakimbilia nje ya nchi kujificha wakikwepa mkono wa sheria.
Alisema baadhi
ya majangili walisalimisha silaha zao kwa hiari na
alitoa pongezi
kwa wajumbe wa kikosikazi, Jeshi la Polisi, kamati za
ulinzi na
usalama za wilaya, mkoa na wananchi.
Profesa
Maghembe, alisema Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi kwa wanyamapori dhidi
ya ujangili na biashara haramu ili kukomesha
vitendo haramu.
Aliliomba Bunge
liidhinishe Sh bilioni 148 na kati ya fedha hizo, Sh bilioni 96.9 kwa ajili ya
matumizi ya kawaida na Sh. bilioni 51.8 kutekeleza miradi ya maendeleo.
Bajeti hiyo
imeongezeka kwa Sh bilioni 12.80 sawa na asilimia 9.4
ikilinganishwa
na bajeti ya 2016/17 na bajeti ya maendeleo imeongezeka kutoka Sh bilioni 17.74
mwaka 2017/18 hadi
Sh bilioni
51.80.
0 comments:
Post a Comment