Dotto Mwaibale
WANANCHI wameomba bajeti ya mwaka ujao
wa fedha ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
iongezwe kwa kuzingatia ukubwa wa wizara hiyo.
Wakizungumza Dar es Salaam jana kwenye
semina ya siku moja iliyoandaliwa na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) ya
kupitia bajeti hiyo ili kuona vipaumbele vyake, waliomba iongezwe ili
kukabiliana na changamoto za wizara hiyo ambayo imelemewa kutokana na ukubwa
wake.
Kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 Wizara hiyo
ilitengewa bajeti ya Sh bilioni 845 ikilinganishwa na mwaka wa fedha wa 2017/18
ambapo jumla kuu ya fedha zote zinazoombwa kwa Wizara hiyo ni Sh.
1,115,608,772,090.
Akizungumza kwenye semina hiyo, Neofita
Kunambi alisema katika Wizara hiyo kuna changamoto kubwa na bila kuongezwa
fedha hazitakwisha.
"Bila ya kuongeza bajeti katika Wizara
hii, wajawazito wataendelea kujinunulia vifaa vya kujifungulia, tunaomba jambo
liangaliwe kwa karibu," alisema Kunambi.
Anna Sangai alisema huduma za afya
zinapaswa kuboreshwa kuanzia upatikanaji wa dawa na vifaa tiba na bila
kuongezwa bajeti katika Wizara hiyo itakuwa ndoto.
Mkazi wa Mbezi Beach, Sadick Juma
alisema upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, miundombinu na ukatili wa kijinsia ni
changamoto kubwa katika Wizara hiyo.
Alisema licha ya kuwepo duka la Bohari Kuu
ya Dawa (MSD) katika Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Muhimbili (MNH),
upatikanaji wa dawa umekuwa mgumu, hivyo kuifanya Muhimbili kuwa na majengo
mazuri bila dawa.
"Ukitaka kuona changamoto hata
ukiwa mwanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ugua au uwe na
mgonjwa ambaye ni mwanachama uende katika hospitali hiyo, kwanza kupokewa tu
pale Mapokezi ni balaa na ukifika muda wa kutakiwa kupata dawa utaambulia
panado na kuambiwa dawa hazipo," alisema Juma.
Juma aliongeza kuwa huduma ya bure kwa
watu wenye misamaha hiyo ni ndoto kwani wagonjwa hao hawasikilizwi kabisa jambo
ambalo ni hatari.
Alisema Serikali imekuwa ikitamba kuboresha
huduma za afya, lakini hali halisi haiko hivyo, akitolea mfano kwa nchi nzima
maduka ya dawa ya MSD kuwa manane tu hivyo upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kutokidhi
mahitaji.
Janeth Mawinza alitaka bajeti hiyo
iangalie zaidi jinsi ya kutibu magonjwa kama homa ya ini ambayo matibabu yake
nchini hayapatikani mpaka dawa itoke India.
Moses Benard alisema ikiwa mjamzito aliye
mjini anatakiwa kujinunulia vifaa vya kujifungulia hali ikoje kwa wa kijijini mwenye
changamoto ya kukosa fedha na kukimbiwa na mwenzake, hivyo kuomba Waziri wa Wizara
hiyo kutoa tamko rasmi la kutaka wajawazito kutonunua vifaa hivyo wanapokwenda
kujifungua.
0 comments:
Post a Comment