Mashaka Mgeta
Chrysostom Rweyemamu |
MWAKA 2006 nilipojiunga katika kampuni ya New Habari House (2006)
Limited, nikiajiriwa kuliandikia gazeti la Mtanzania, nipo nilipokuwa karibu na
mmoja wa waandishi nguli wa habari nchini, Chrysostom Rweyemamu.
Mei 28, mwaka huu, Rweyemamu aliyekuwa pia Mjumbe wa Bodi na
Katibu mstaafu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), alifariki
akiwa amelazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es
Salaam.
Wapo wanaoweza kukiona kipindi cha kuanzia 2006 nilipomfahamu
Rweyemanu hadi sasa ni miaka michache. Hawatakuwa wamekosea kutokana na ukweli kwamba
tafsiri ya namba inatokana na ufafanuzi wa anayejenga hoja.
Lakini pia katika utumishi wangu, sikudumu kwa muda mrefu kwenye
kampuni hiyo. Nilifanya kazi kwa takribani mwaka mmoja, nikarejea katika
kampuni ya The Guardian Limited niliyokuwapo kabla ya kujiunga New Habari House
(2006) Limited.
Bado kuwapo katika kampuni hiyo kwa kipindi cha takribani mwaka
mmoja kinaweza kuonekana kuwa kifupi. Dhana hiyo inaweza kuwa sahihi kutokana
na hoja inayojengwa na mtu anayeamini hivyo.
Hata hivyo, kuwa kwangu karibu naRweyemamu hakukuwa ndani ya
kampuni hiyo pekee, bali katika ziara kadhaa zilizoandaliwa na JET kwenda
kwenye maeneo tofauti ya nchi, kutathimini na kuandika habari zinazohusiana na
mazingira.
Ninakumbuka katika ziara hizo, ukiacha maelekezo ya kitasnia,
Rweyemamu alifahamika zaidi kwa utani uliotokana na kupenda kwake kutumia
pilipili iluyowekwa kwenye chakula. Alipenda kutumia pilipili yenye ganda jekundu.
Ndio maana tulipofika hotelini, aliulizia aina ya pilipili
iliyopo. Wakati mwingine alilazimika kwenda kununua pilipili nyekundu, ili
mradi kukidhi hitaji lake.
Ziara hizo zinaweza kutafsiriwa kufanyika katika siku chache.
Anayetafsiri hivyo anaweza kuwa sahihi kwa kadri anavyozifafanua hesabu zake na
sababu zake.
Ingawa ni hivyo, ukweli unabaki kwamba mimi ni miongoni mwa watu
hususani waandishi wa habari waliobahatika kukaa, kufanya kazi, kula na kunywa pamoja
na Rweyemamu.
Katika siku zangu za awali kujiunga New Habari House (2006)
Limited, tofauti ya kwanza niliyoiona na mahali nilipotoka, yaani The Guardian
Limited ni kuwapo kwa mafunzo ya ndani kwa waandishi wa habari.
Kwa kawaida, waandishi wa habari hukutana asubuhi kwenye chumba
ama eneo maalum ndani ya chumba cha habari, kusoma, kujadili, kutathmini na kufanya
ulinganifu wa habari zilizotolewa na chombo chao, ikilinganishwa na ilivyo kwa
vyombo vingine.
Kisha waandishi hushiriki kutoa mawazo ya habari mpya, namna ya
ukusanyaji wa taarifa, vyanzo vya kupatikana kwake (taarifa) na mambo mengine
yanayohusu ratiba ya siku husika.
Lakini kwa New Habari House (2006) Limited hali hiyo ilikuwa
tofauti kidogo. Kwamba kila Ijumaa hapakuwa na patio la magazeti, bali
waandishi walikusanyika kwenye chumba mahususi kwa ajili yakushiriki semina
fupi ya kukumbushana mambo ya kuzingatia katika uandishi wa habari.
Darasa hilo liliratibiwa na kuongozwa na Rweyemamu tunayeomboleza
kifo chake sasa. Rweyemamu alimudu kutumia taaluma na uzoefu wake katika tasnia
ya habari kufundisha, kukumbusha na kuelekeza namna bora ya kuandika habari
zenye maslahi kwa umma.
Rweyemamu alikuwa muumini mzuri wa matumizi sahihi ya lugha hasa
za Kiswahili na Kiingereza. Licha ya kuchapisha gazeti la Mtanzania, New Habari
House (2006) Limited ilikuwa (nafikiri hadi sasa) ikichapisha gazeti la The African
kwa Kiingereza.
Namna bora ya ufundishaji, uelekezi na ushirikishi wa Rweyemamu
kupitia darasa hilo, yalinifanya nijione ‘kiumbe mpya’ katika tasnia ya habari,
nikipata ujuzi zaidi, uelewa zaidi na ufahamu zaidi kuhusiana na masuala
mbalimbali ya uandishi wa habari.
Ninatambua na wengine wengi wanaweza kulikubali hili, kwamba
katika utendaji kazi wa uandishi wa habari, ni rahisi kugundua na kukosoa upungufu
kadha wa kadha unaotokea, ukifanywa na waandishi wa habari.
Ndivyo ilivyokuwa kwa Rweyemamu katika uhai wake. Alikuwa mwepesi
wa kubaini upungufu katika uandishi wa habari kwa magazeti ya ndani ya New
Habari House (2006) Limited nay ale yaliyokuwa yanachapishwa na kampuni washindani.
Ni kutokana na hali hiyo, nilijifunza na kupata uelewa mpana zaidi
katika masuala ya uandishi wa habari hasa wa kivitendo kutoka kwa Rweyemamu
aliyekuwa Mhariri, Mwalimu, muelekezi na msimamizi bora wa mafunzo ya ndani ya
chombo cha habari.
Katika kuonesha dhamira nzuri ya kuleta mageuzi na mabadiliko
chanya, Rweyemamu aliweka mfumo unaotoa fursa kwa kila mwandishi wa habari
kunufaika kutokana na mafunzo hayo.
Mfumo huo ulihusisha kuwapo orodha maalum ya mahudhurio
aliyoisimamia na kuhakikisha kwamba mafunzo ya ndani yanakuwa sehemu ya vigezo
muhimu vya ushiriki wa mwandishi wa habari katika ajira yake.
Nilipenda kuwapo kazini kila siku kwa kadri ya hitaji la ajira
yangu, lakini nilipenda zaidi kufika ofisi kila Ijumaa ili nisikose kipindi cha
mafunzo yaliyotolewa na Rweyemamu.
Ndio maana, hata niliporejea The Guardian Limited baada ya
takribani mwaka mmoja, miongoni mwa mambo niliyohisi kuyakosa, nikabaki ninayakumbuka
ni kipindi cha mafunzo ya ndani kilichokuwa kinaongozwa na Rweyemamu.
Hata nilipokutana naye kwenye ziara za JET, Rweyemamu alikuwa na
hulka ya kushirikiana na washiriki wote, waandishi wabobezi na hata waliochipukia
katika tasnia hiyo.
Hakuwa na ‘uchoyo’ wa kutaka aonekane kuandika makala bora kuliko
wengine, bali alishirikishana na waandishi wengine na kujadiliana masuala ya
muhimu yaliyoibuka wakati wa ziara.
Ni nadra kuzikuta karama hizo kwa waandishi wengi ndani ya mataifa
yanayoendelea, lakini Rweyemamu aliiishi hali hiyo na kuacha kizazi cha
waandishi bora wa habari, wakiwamo wale waliopitia taasisi ya mafunzo ya
uandishi wa habari ya Maarifa (Mamet) iliyokuwa chini ya kampuni hiyo.
Mwenyezi Mungu ampumzishe katika usingizi wa amani Chrysostom
Rweyemamu-AMINA
0 comments:
Post a Comment