Joyce Kasiki, Dodoma
George Simbachawene |
SERIKALI itawachukulia
hatua wakurugenzi wa halmashauri ambao hawajawalipa fedha za uhamisho za
watumishi hususan walimu kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi.
Akijibu swali la
Mbunge wa Viti Maalumu, Kemilembe Lwota (CCM) bungeni jana, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George
Simbachawene, alisema kuna tabia ya baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri kuhamisha
watumishi hasa walimu kwa kuwakopa.
Katika swali
lake, Lwota alitaka kujua kauli ya Serikali kuhusu lini italipa watumishi
stahiki zao.
“Nilishasema
hadi Aprili 30, wanapaswa kuwa wamelipa walimu waliowahamisha na hili
nililisema si kwa madeni ya nyuma ya uhamisho tumepeleka Wizara ya Fedha
kulipwa.
“Lakini kuna
uhamisho wa kati ya Januari na Machi kwa kupanga ikama za walimu. Siku ya
mwisho imefika, Serikali itachukua hatua kwa ambao hawajalipa watumishi
waliowahamisha,” alionya Simbachawene.
Alibainisha kuwa
haiwezekani Serikali ipambane kupunguza madeni lakini watu wanakuwa viwanda vya
kuzalisha madeni yasiyo na sababu," alisema Simbachawene.
Aidha, alisema
suala hilo limewekewa msisitizo na Serikali na sasa upo mkakati wa kuandaa
fedha kwa ajili ya kupanga ikama kwenye halmashauri zote na malipo ya uhamisho
yawe ya moja kwa moja kwa watumishi watakaohamishwa.
Awali katika
swali la msingi, Mbunge huyo alitaka kujua lini Serikali itawalipa stahiki zao
watumishi wa wilaya ya Buchosa ambako watumishi 98 walihamishwa kutoka wilaya
mbalimbali lakini hawajalipwa fedha za uhamisho.
Akijibu swali
hilo, Naibu Waziri Seleman Jafo alisema halmashauri hiyo ni miongoni mwa mpya
na iligawanywa kutoka wilaya ya Sengerema.
Alikiri kuwa
watumishi wa Sengerema, Ilemela, Jiji la Mwanza, Kwimba na Magu wanadai Sh
milioni 354 na tayari Sh milioni 44.5 zimelipwa kwa watumishi 16.
“Hadi Desemba
mwaka jana Halmashauri imebakiza madeni ya uhamisho kwa watumishi 88 ya jumla
ya Sh milioni 292.5 na madeni yaliyobaki yamewasilishwa Wizara ya Fedha kwa
ajili ya uhakiki ili yalipwe,” alisema.
0 comments:
Post a Comment