Frank Mvungi, Maelezo
SERIKALI imewahakikishia wananchi kuwa
dawa zilizopo katika soko zina ubora kwa asilimia 98 na itahakiksha zinaendelea
kukidhi vigezo vya ubora kama zilivyokuwa wakati zinasajiliwa kwa mujibu wa sheria,
kanuni, miongozo na taratibu za udhibiti.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Hiiti Sillo wakati wa mkutano na
waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam.
“Katika maabara ya TFDA inayokidhi ithibati
ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kati ya sampuli za dawa 199 za binadamu
zilizochunguzwa, sampuli 184 sawa na asilimia 92.5 zilikidhi vigezo vya ubora
na sampuli za dawa 10 aina ya Ergometrine ya sindano ambayo ni sampuli 5 sawa
na asilimia 2.5 hazikufikia ubora kwa kuwa na kiasi cha kiambata hai chini ya
kiwango kinachokubalika.” alisisitiza Sillo
Alifafanua kuwa kabla ya dawa kusajiliwa
na TFDA na hatimaye kuruhusiwa kuingia katika soko, zinafanyiwa tathmini ya ubora,
usalama na ufanisi sanjari na ukaguzi wa mifumo ya utengenezaji bora kiwandani
na hizo ni hatua za awali za mifumo ya udhibiti wa dawa duniani.
Pia Sillo aliongeza kuwa dawa zinapokuwa
katika soko zinafuatiliwa na TFDA kuona kama zinaendelea kukidhi vigezo vya
ubora hadi tarehe ya mwisho ya matumizi (expiry date) ambapo utaratibu huu
hujulikana kama Post- Marketing Surveillance au Market Control kwa mujibu wa
mwongozo wa shirika la Afya Duniani (WHO) na ulianza kuwekwa na TFDA tangu
mwaka 2007.
Katika utaratibu huo kila mwaka sampuli
za dawa za aina tofauti zinachukuliwa na wakaguzi kutoka katika soko
Zahanati,Vituo vya Afya, Hospitali,maduka ya dawa na maghala ya kuhifadhia dawa
ya umma na binafsi na kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara.
Vigezo vinavyotumika kuchagua dawa
zinazofanyiwa ufuatiliaji ni pamoja na dawa zenye matumizi makubwa,dawa za
kutibu magonjwa ya makundi maalum kama watoto na akina mama wajawazito,dawa
zenye historia ya kushindwa kustahili mazingira mbalimbali ya usafirishaji na
utunzaji (unstable products)
Kwa kipindi cha mwaka 2012/2015 Sillo
alibainisha kuwa dawa zilizofanyiwa
ufuatiliaji ili kuona ubora wake ni pamoja na dawa za kutibu malaria,dawa aina
ya vijiua sumu (Antibiotics) Dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi,dawa za kupunguza
maumivu,dawa za kutibu kisukari,dawa za kutibu magonjwa ya moyo,dawa za kuzuia
kutoka damu nyingi wakati wa kujifungua aina ya misoprostol.
Katika kipindi cha mwaka 2016/2017 hadi
machi 2017, TFDA ilifuatilia katika soko,ubora wa dawa za binadamu aina ya
Albendazole vidonge,mchnaganyiko wa dawa ya vidonge aina ya Diclofenac na
paracetamol,dawa ya macho yenye mchanganyiko wa Dexamethazone na Neomycin,dawa
za mifugo aina ya Oxytetracycline 10% na 20 ambazo uchunguzi wake uko katika
hatua za mwisho na matokeo yatatolewa mara yatakapokuwa tayari.
Aidha Sillo amesema kuwa mfumo wa
kufuatilia usalama wa dawa katika soko unafanya kazi vizuri hapa nchini tangu
mwaka 1989 na umeendelea kuboreshwa ambapo oktoba 2016 tulianzisha mfumo wa
utoaji taarifa za madhara ya dawa kielekroniki kwa kutumia simu ya kiganjani.
Mamlaka ya Chakula na Dawa
Tanzania(TFDA) kwa mujibu wa Sheria ya Chakula,Dawa na Vipodozi,sura ya 219 ina
jukumu la kudhibiti ubora na usalama wa chakula,dawa, vipodozi na vifaa tiba
ili kulinda Afya za wananchi.
0 comments:
Post a Comment