Hussein Ndubikile na Grace Gurisha
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam limetaja sababu tatu za kumkamata aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha na
Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima, katika tukio lililombatana na kufyatua risasi
tatu angani.
Mtuhumiwa huyo jana alifikishwa kwenye
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kujibu tuhuma zinazomkabili na
kutetewa na Wakili Peter Kibatala.
Hatua hiyo imekuja baada ya kusambaa mitandaoni
picha za video zikionesha gari aina ya Toyota Land Cruiser namba T 296 ATW,
ambalo liliegeshwa pembeni karibu na hoteli ya Double Tree, Masaki, Dar es
Salaam, wakashuka askari wawili – mmoja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na
mwingine polisi wa kawaida.
Akizungumzia suala hilo jana, Kamanda wa
Kanda hiyo, Simon Sirro alisema tukio hilo lilitokea juzi saa sita mchana
Masaki karibu na ofisi za Ubalozi wa Canada, ambapo mfanyakazi wa kampuni ya
Priscane Business Enterprises, alikuta gari la Malima limeegeshwa sehemu isiyotakiwa,
huku akisisitiza dereva wa gari alipotakiwa alipeleke gari hilo yadi alikaidi
na kulirudisha kwa nguvu lilipokuwa.
“Mfanyakazi wa Priscane alilikuta gari
la Malima likiwa na dereva aliyeambiwa ameegesha sehemu isiyoruhusiwa, lakini cha
kushangaza alikaidi ndipo mvutano ukaanza kati yake na mfanyakazi huyo na kulazimu
polisi kuingilia kati,” alisema Kamanda Sirro.
Katika video ya tukio hilo, askari wa
FFU baada ya kushuka kwenye gari hilo alionekana akinyanyua bunduki na kufyatua
risasi angani, kabla mwenzake kumfuata na kumshika kifuani na kutaka kumrudisha
kwenye gari.
Tukio liliendelea kwa askari aliyemfuata
mwenzake kumfuata Malima na kuzungumza naye, lakini wakati wakiendelea na
mazungumzo, yule askari aliyefyatua risasi pia alimfuata na kumsukuma mara
mbili waziri huyo wa zamani, kisha kuinua juu bunduki na kusikika akitamka:
“Kwa nini hamheshimu Serikali nyie, mzee
heshimu Serikali, mimi nimewekwa kuitumikia Serikali, siwezi kudharaulika.”
Katika video hiyo pia ilisikika sauti ya
mtu ambaye hakuonekana akitamka: “Huna
mamlaka, huna mamlaka ya kutishia.”
Wakati hayo yakiendelea, Malima
alionekana kujibizana na askari hao akiwa ameweka mikono mfukoni mwa suruali
yake, huku mmoja wa askari hao aliyeonekana akimsihi mwenzake aende kwenye gari
akitamka: “Poti, Poti, Poti ee!”
Katika mkutano wake na wanahabari, Kamanda
Sirro alisema Malima alipotoka nje ya Ubalozi huo, askari walimwambia gari lake
linatakiwa liende yadi kwa sababu lilikiuka sheria za maegesho, lakini
alionekana kukaidi hali iliyolamzimu askari huyo kufyatua risasi tatu angani.
Alisema licha ya amri ya askari, Malima
aliendelea kukaidi huku akitamka kuwa yeye amefanya kazi na viongozi wakubwa,
hali iliyomlazimu askari kufyatua risasi nyingine.
Sirro alisema: “Kelele za watu waliokuwa
wakizomea, zilichangia askari kutumia busara kupiga risasi hizo angani ili kuwatawanya
na endapo wangewaacha Malima na dereva wake, ingechangia
kuwaaminisha wananchi kuwa polisi wameshindwa kufanya kazi yao.”
Alitaja sababu nyingine kuwa ni
mazingira hatarishi yaliyomlazimu askari huyo kufyatua risasi, kulingana na
wakati na kwamba askari wangeondoka eneo la tukio bila kuwakamata, wangeshitakiwa
kwa woga.
Aidha, alisema waziri huyo wa zamani alifikishwa
mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili yakiwamo ya kuzuia polisi kufanya
kazi zao, kujeruhi na kukaidi amri.
Mahakamani
Malima na dereva wake, Ramadhani Kingwande
walipandishwa kizimbani kujibu mashitaka ya kuzuia polisi kufanya kazi yake na
kujeruhi.
Kesi hiyo inawakutanisha Wakili Kibatala
na Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono.
Wakili Mwanaamina alidai mbele ya Hakimu
Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage kuwa Malima ambaye alikuwa Mbunge wa
Mkuranga na dereva wake wabnakabiliwa na
mashitaka mawili.
Ilidaiwa kuwa washitakiwa hao walitenda
makosa hayo Mei 15 Masaki Kinondoni, Dar es Salaam.
Wakili huyo alidai kuwa Kingwande kwa
nia ya kukataa kukamatwa kutokana na kuegesha vibaya gari lake namba T 587 DDL,
alimjeruhi Mwita Joseph ambaye ni Ofisa Operesheni wa kampuni ya Priscane
Business Enterprises na kumsababishia maumivu makali.
Wakili huyo alidai kuwa Malima alitenda
kosa la shambulio, Mei 15 Masaki, wakati akimzuia dereva wake kukamatwa
baada ya kutuhumiwa kutenda kosa barabarani.
Ilidaiwa kuwa siku hiyo, Malima alimzuia
askari Polisi namba H 7818 Konstebo Abdu kufanya kazi halali ya kumkamata Kingwande
aliyefanya makosa ya kumshambilia Joseph.
Washitakiwa walikana mashitaka hayo na
upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi haujakamilika na hawana
pingamizi la dhamana.
Wakili Kibatala aliiomba Mahakama kutoa
masharti nafuu ya dhamana kutokana na asili ya mashitaka hayo.
Pia alidai Malima ambaye ni mshitakiwa
wa pili katika kesi hiyo ni mtu anayetambulika katika jamii kwa kuwa alikuwa
Mbunge na Naibu Waziri.
Hakimu Mwijage aliwataka washitakiwa
kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini dhamana ya Sh milioni tano.
Washitakiwa hao waliachwa huru baada ya kutimiza masharti ya dhamana. Kesi iliahirishwa
hadi Juni 15.
Hata hivyo, Wakili Kibatala alidai
mahakamani hapo kuwa katika tarehe ijayo atawasilisha pingamizi kwamba
mashitaka ya pili yanayomkabili Malima hayaendani na maelezo yake.
0 comments:
Post a Comment