SAKATA la fedha zilizochangwa kwa ajili ya kuwafariji
wafiwa wa watoto,walimu na dereva wa Shule ya Lucky Vincent ya Arusha
waliofariki katika ajali kutumika katika
matumizi mengine limetinga bungeni huku wabunge wakilaani.
Suala hilo limeibuka jana baada ya kipindi cha maswali na
majibu ambapo Mbunge wa Ukonga,Mwita Waitara (Chadema) alitaka kupata mwongozo
wa Mwenyekiti Andrew Chenge aliyekuwa anaongoza mkutano huo kuhusiana na
taarifa ya fedha za rambirambi kupelekwa kukarabati hospital ya Mount Meru iliyopo
Arusha.
‘’Mheshimiwa Mwenyekiti naomba mwongozo wako kwa kutumia
kanuni ya 68 (7) inayohusu jambo lilijitokeza mapema bungeni,Nilikuwa hapo nje
nimeangalia magazeti yanaelezea matumizi ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya
rambirambi na kuwafariji wafiwa wa watu waliofariki katika ajali ya shule ya
Lucky Vincent zimetumika kinyume na malengo yake’’alisema Waitara na kuongeza
kuwa
“Madaktari wamelipwa kama posho na fedha zingine zinakarabati hospitali ya Mount Meru tofauti
na ilivyokusudiwa,katika hili bunge
linahusika kwa maana tulikatwa posho hapa ili kusaidia familia za
wafiwa,ilikuwa misaada klwa wahusika sasa hii tabia imekuwa ikijirudia.”
Alisema watu wamekuwa wakichanga kwa ajili ya kusaidia
watu wanaopata matatizo lakini serikali imekuwa haifikishi fedha hizo kwa
wahusika,tabia hiyo imekuwa ikijirudia
mara kwa mara jambo ambalo si zuri kwani watu wataacha kuchanga wakijua
kwamba fedha hazisaidii walengwa.
“Tabia hii inanikera hata mimi mwenyewe kama tutakuwa
tunachanga fedha za rambi rambi alafu inabadilishwa matumizi juu kwa juu bila
hata wahusika kupelekewa,kama ni hivyo ni vyema kila chama kikakusanya fedha za
michango wenyewe au kada zingine zifanye hivyo kwa lengo la kuwafikishia
wahusika wenyewe ili kuepuka ulaji wa fedha za michango’’
Akijibu mwongozo huo,Chenge alisema “Kwa mila na desturi
za kiafrika ukishatoa mchango wako wa rambi rambi unawaachia familia ile au
chombo kile,sijatoa mwongozo haya ni maoni yangu,naomba tusiendeleze jambo
hilo,serikali ipo bunge lipo unategemea mrejesho ili siku nyingine mkiombwa iwe
rahisi kutoa lakini kuleta tuhuma tu sio”
“Ila kwa mwongozo wangu swala lako halijatokea mapema
bungeni leo kwahiyo sina cha kulijibia,hatuendeshwi na magazeti humu bungeni.”
Mchango uliotolewa na bunge kwa ajili ya kuwafariji
wafiwa ni milioni 100 ,michango ya jumla iliyotolewa na wadau ni zaidi ya
milioni 300 ambapo fedha zilizotolewa kwa familia za wafiwa ni zaidi ya
shilingi milioni 133 ambazo katika
wafiwa 35 kila familia ilipata shilingi milioni 3.8.
0 comments:
Post a Comment