PARIS, Ufaransa
Emmanuel Macron |
EMMANUEL Macron usiku wa kuamkia jana
aliahidi ‘kuilinda Ulaya’, dakika chache baada ya kuwa kiongozi kijana kuliko
wote wa Ufaransa tangu enzi za Napoleon.
Macron (39), alimshinda mgombea wa chama
cha National Front (FN), Marine Le Pen (48), katika uchaguzi ambao unagusa
mustakabali wa Ulaya.
Awali alishatangaza kwamba hataunga
mkoono Uingereza kujitoa kwnye Umoja wa Ulaya na hata kuuita uamuzi huo wa
Uingereza kuwa ni ‘jinai’.
Baada ya kura kuhesabiwa jana asubuhi,
Macron alizoa asilimia 66.1 ya kura katika uchaguzi huo ambao kwake ni wa
kwanza kushiriki, akiwa amemwacha kwa mbali Le Pen aliyepata kura 33.9.
Asilimia 74.62 ya waliojiandikisha ndio
walijitokeza kupiga kura, lakini kwa mshangao wa wengi, theluthi moja
hawakujitokeza au hawakuandika chochote kwenye karatasi ya kura.
Dakika 15 baada ya matokeo kutangazwa,
Le Pen alikubali kushindwa na kusema alimpigia Macron simu ‘kumpongeza’ kwa
ushindi wake.
Baadaye jioni, Macron alihutubia maelfu
ya wafuasi wake ambao walikusanyika nje ya jengo la Louvre katikati ya Jiji.
“Tulichokifanya kwa miezi mingi, kila
mtu alidhani kisingewezekana, lakini hawakuijua Ufaransa. Nakushukuruni kwa imani
yenu. Ahsanteni kwa baadhi yenu kuthubutu.”
Macron pia aliwazungumza waliompigia kura
Le Pen, akisema: “Wameonesha hasira zao leo. Nawaheshimu na nitafanya kila
ninachoweza katika miaka mitano ijayo kuhakikisha kwamba hapana sababu ya kuchagua
wenye siasa kali. Leo kuna Ufaransa. Ufaransa uliyoungana tena.”
Alisisitiza akisema kazi iliyo mbele
yake ni ‘nzito’ na kuongeza kuwa Ulaya na dunia kwa jumla, wanaiangalia
Ufaransa. Aliongeza kwamba atafanya kazi ya “kuibadilisha Ulaya yetu”.
Macron alisema Ufaransa imechagua “ujasiri”
na kuahidi kuitumikia nchi yake kwa “nguvu na unyenyekevu” mkubwa.
Mkewe Brigitte Trogneux ambaye alipata
kuwa mwalimu wake, anatarajiwa kubeba jukumu kubwa ndani ya serikali mpya yenye
mrengo wa kati.
Akitumia mtazamo wa Michelle Obama
kutumika kama mke wa rais, Brigitte (64) ambaye anamzidi mumewe miaka 24,
anaripotiwa kuwa atajihusisha zaidi na masuala ya elimu.
Akiwa na miongo miwili ya uzoefu kuliko
mumewe na kupata kuwa mwalimu wake mwenye mchango mkubwa katika kujenga tabia
yake akiwa na umri wa miaka 15, bibi huyo wa wajukuu wanane anatarajiwa kubeba
jukumu kubwa serikalini.
“Nia kuu ya Brigitte ni kufanya mageuzi
katika elimu na atajikita zaidi kuhudumia watoto wenye usonji na waishio katika
mazingira magumu nje ya siasa,” mwandishi mwenza wa wasifu wa wanandoa hao,
Candice Nedelec aliiambia Sunday Times.
Wakati Macron akifanya kazi kama Waziri
wa Fedha chini ya Rais Francois Hollande, Brigitte alikuwa anafuatilia shajara
ya mumewe lakini pia akisahihisha hotuba zake.
0 comments:
Post a Comment