LONDON, Uingereza
Malkia wa Uingereza aikiwa na mumewe |
MUME wa Malkia wa Uingereza, Prince
Philip ametangaza kustaafu shughuli za kifalme baada ya kufikisha umri wa miaka
95 na Malkia Elizabeth ameunga mkono uamuzi huo, ilielezwa jana.
Kustaafu huko kwa Mwana wa Mfalme wa
Edinburgh mwenye umri wa miaka 95 sasa, kulitangazwa jana kwenye mkutano wa
faragha ulioitishwa kwenye makazi ya Malkia ya Kasri ya Buckingham.
Wafanyakazi wote wa ufalme nchini kote
waliitwa jijini hapa jana, na kusababisha wasiwasi duniani kote juu ya afya ya
Malkia na mumewe.
Lakini baadaye ilikuja kubainika kwamba
Philip-mume wa Malkia aliyekaa kipindi kirefu katika historia-ameamua kuachana
na majukumu yake ya kifalme baada ya kumsaidia mkewe kwa miaka 70.
Malkia ataendelea na majukumu yake kama
ambavyo amekuwa na alivyoapa kuitumikia nchi yake kwa maisha yake yote.
Taarifa iliyotolewa jana asubuhi kwenye
kasri la Buckingham ilisema: “Mtukufu Mwana wa Mfalme wa Edinburgh ameamua kwamba
hatashiriki shughuli zote za umma kuanzia kipindi cha kupukutika majani mwaka
huu. Katika kufikia uamuzi huo, Mwana huyu wa Mfalme anaungwa mkono kwa
asilimia 100 na Malkia.
“Mwana wa Mfalme wa Edinburgh ni Mlezi,
Rais au mwanachama wa zaidi ya mashirika 780, ambamo ataendelea kushiriki,
ingawa hatajitokeza sana kushiriki shughuli mbalimbali.”
Pamoja na umri wa miaka 95, Philip
amewazidi vijana wengi miongoni mwa vizazi vya kifalme ambapo mwaka jana tu
alishiriki shughuli rasmi 219 nchini, akiwazidi Prince William, Mke wa Mwana
wa Mfalme wa Cambridge na Prince Harry
kwa pamoja.
Ujumbe uliotumwa usiku wa kuamkia jana
ulibainisha kwamba wasaidizi waandamizi wa Malkia waliita wafanyakazi wote wa
kifalme nchini kote kuja jijini hapa kwa ajili ya kikao cha jana saa 4 asubuhi
kabla ya kutolewa tamko hilo.
Baada ya hisia na wasiwasi juu ya afya
ya Prince Philip, ilikuja kubainika kwamba ana siha njema lakini anastaafu
baada ya kufikisha umri wa miaka 95.
0 comments:
Post a Comment