Mwandishi Wetu
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka askari Polisi
wanawake kutoka Shirikisho la Majeshi la Polisi Kusini mwa Afrika (SARPCCO) kushiriki
kikamilifu oparesheni za kijeshi zinazofanyika kwenye ukanda huo kukabiliana na
uhalifu.
Samia alitoa kauli hiyo alipofungua mafunzo ya siku tatu
ya polisi wanawake kutoka nchi wanachama wa SARPCCO Dar es Salaam jana.
“Vyeo haviji tu ni lazima polisi wanawake muoneshe
mnaweza, ili muweze kupandishwa vyeo na kupata nafasi za uongozi kwenye majeshi
yenu. Mshiriki operesheni za kijeshi Kusini mwa Afrika,” alisema Samia.
Aliwaambia muda wa kulalamika kuwa hawapandishwi vyeo umepitwa
na wakati na sasa lazima wachape kazi na kuonesha wanaweza majukumu
wanayopangiwa ili wapande vyeo.
Kuhusu utendaji kazi wa polisi wanawake, Makamu wa Rais
aliwataka kutumia mkutano huo kujadili kwa kina namna ya
kuondoa changamoto zinazorudisha nyuma utendaji kazi wao.
Alisema kama polisi wanawake wataacha majungu na kujenga
umoja na mshikamano miongoni mwao, watafikia malengo yao haraka hasa katika
kushiriki kikamilifu mapambano dhidi ya uhalifu ikiwamo biashara ya dawa za
kulevya.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alisema ana
imani mafunzo hayo yatasaidia polisi hao kuimarika ipasavyo katika utendaji kazi
wao.
Aliwahimiza polisi hao wanaopata mafunzo hayo kwenda
kuelimisha wenzao mipango na mikakati waliyoweka ya kulinda raia na mali zao nchini
mwao.
0 comments:
Post a Comment