IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR
Dk Abdalla Juma Saadala |
WANANCHI visiwani vya Zanzibar wameshauriwa
kuendeleza kwa vitendo utamaduni wa uzalendo wa kusaidiana wakati wa
yanayotokea nchini bila kujadili tofauti za kisiasa na kidini.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu
wa CCM Zanzibar, Dk Abdalla Juma Saadala, “Mabodi”mara baada ya ujenzi wa nyumba
ya Balozi wa Nyumba kumi Asha Abdalla Baruti iliyobomoka kutokana na maafa ya
mvua zinazonyesha maeneo ya Fuoni Migombani.
Dk Mabodi alisema maafa yanapotokea
hayachagui sehemu ya kuathiri bali yanawakumba wananchi wote hivyo ni muhimu
wanajamii kushirikiana kwa mambo ya kijamii na kimaendeleo na kuacha siasa za
utengano na chuki.
Ujenzi huo umefanyika kutokana na agizo
la Naibu Katibu Mkuu huyo alipowataka uongozi wa CCM na UVCCM Wilaya ya Dimani
Unguja, kumjengea makaazi ya muda mwananchi huyo ambaye hakuwa na sehemu ya
kuishi kutokana na nyumba yake kuharibiwa na mvua zilizonyesha hivi karibuni.
Alisema hatua ya Chama hicho kutoa msaada
na kushiriki katika masuala ya shughuli za kijamii kwa wananchi itakuwa ni
utamaduni endelevu kwa Unguja na Pemba.
Alieleza kwamba lengo la CCM kutoa
msaada wa kujenga makaazi ya dharura kwa wananchi wakati wa kipindi hichi cha
maafa ni kuendeleza kwa vitendo siasa za waasisi wa vyama vya ASP na TANU ambao
walishiriki katika masuala mbali mbali ya kitaifa na kimataifa kwa lengo la
kuwa karibu na wananchi waliowapa ridhaa ya uongozi.
Pia alisema wakati wa Kampeni za
Uchaguzi CCM ilikuwa ikienda kwa wananchi katika maeneo mbali mbali kuomba kura
za kuiweka madarakani hivyo hata kwa kipindi cha maafa na changamoto
zinazoikabili jamii ni lazima kirudi kwa wananchi kuwaunga mkono na kuwafariji
kwa vitendo.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema CCM ya
sasa Viongozi wa ngazi mbali mbali ndani ya Chama na Serikali kurudi kwa
wananchi kujua changamoto zinazowakabili na kuzifanyia kazi kwa wakati ni jambo
la lazima na sio la hiari.
“Nasaha zangu kwa wananchi ni kwamba
pindi yakitokea maafa hasa magfuriko tusaidiane kwanza kupitia umoja wetu
katika mitaa mbali mbali tunayoishi kwa kuwahifadhi katika maeneo salama
wenzetu wanaopata maafa huku tukisubiri serikali zetu zichukue hatua za kutoa
misaada,” alisema Dkt. Mabodi.
Pamoja na hayo aliwataka vijana nchini
kuwa mstari wa mbele kwa kujitokeza muda wowote kusaidia masuala ya ujenzi wa
miundombinu iliyoharibiwa na maafa ili nchi iweze kujivunia uwepo wa kundi hilo
ambalo ndio nguvu kazi ya taifa.
Pia aliwataka viongozi wa kisiasa nchini
kuondokana na mazoea ya kulalamika na kulaumu serikali hasa katika kipindi
hichi cha maafa na badala yake wawe sehemu ya kuwahamasisha wafuasi wao
wajitolee kuwasaidia watu waliofikwa na maafa huku serikali ikiendelea kutafuta
ufumbuzi wa kudumu wa kutatua tatizo hilo.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Fuoni, Mh.
Yussuf Hassan Iddi amesema jimbo hilo litaendelea kusaidia awamu kwa awamu
wananchi mbali mbali waliopata maafa ili waweze kurudi katika hali yao ya
kawaida.
Alisema uongozi wa jimbo hilo baadae
utahakikisha unajenga nyumba ya kudumu kwa mwananchi huyo ili aweze kupata
uhakika wa makaazi yake.
Kwa upande wake Mbunge Mteule wa Bunge
la Afrika Mashariki kwa tiketi ya CCM, Dkt.Abdulla Hasnuu Makame alisifu hatua
zilizochukuliwa na CCM kwa kuendeleza utaratibu wa kuwafariji wananchi wakati
wa matatizo mbali mbali ya kitaifa .
Aliahidi kuiwakilisha vyema CCM katika
Bunge hilo ili fursa mbali mbali zinazopatikana ziweze kusaidia katika
kuimarisha miradi ya kijamii hasa kuongeza miundombinu ya barabara, Elimu, Afya
na ajira kwa vijana.
Mapema Bi. Asha Abdalla ameishukru CCM
na wananchi wote walioshiriki katika zoezi la kumjengea nyumba yake na kuongeza
kwamba hatua hiyo imemfariji na kumpa nguvu za kuendelea kufanya kazi za
kujipatia kipato kwa ufanisi zaidi.
0 comments:
Post a Comment