*JPM amtaka ajifikirie, ajitathmini na kuachia madaraka
*Ni
miaka miwili tangu alipojiuzulu kwa kashfa ya Escrow
Celina Mathew na Suleiman Msuya
Rais John Magufuli |
MIAKA miwili baada ya Profesa Sospeter
Muhongo kujiuzulu uwaziri wa Nishati na Madini baada ya kuhusishwa na sakata la
uchotwaji wa mabilioni ya fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, huenda
akalazimika tena kujiuzulu baada ya Rais John Magufuli kumtaka afanye hivyo.
Safari hii, Profesa Muhongo atang’oka
baada ya Kamati iliyoundwa na Rais kuchunguza mchanga wenye madini (makinikia) kutoa
taarifa inayoonesha upotevu wa Sh trilioni 1.439 baada ya uchunguzi, kupima
mchanga ulio kwenye kontena 277 zilizozuiwa kusafirishwa nje ya nchi tangu
Machi.
“Profesa Muhongo nampenda sana, pia ni
rafiki yangu, lakini kwenye hili ajifikirie na ajitathmini na bila kuchelewa,
nilitaka aachie madaraka,” alisema Rais Magufuli baada ya kupokea taarifa hiyo
jana Ikulu, Dar es Salaam.
Mbali na Muhongo ambaye ni Mbunge wa Musoma
Vijijini, Rais alitangaza kumsimamisha kazi Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Dominic Rwekaza na kuvunja Bodi ya Wakala
huo.
Pia, aliagiza wafanyakazi wote wa TMAA kuchunguzwa
na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili kubaini waliohusika
na ubadhirifu huo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.
Magufuli alitoa uamuzi huo baada ya Kamati
hiyo aliyoiteua Machi 29 na kuiapisha Aprili mosi, kukamilisha uchunguzi kuhusu
mchanga wenye dhahabu.
Kauli ya Rais Magufuli aliyekiri kuwa na
urafiki wa karibu na Profesa Muhongo ni pigo kwa msomi huyo ambaye Januari 24, mwaka
juzi alimwandikia Rais Jakaya Kikwete barua ya kujiuzulu baada ya kuhusishwa na
Escrow.
Muhongo ambaye wakati huo alikuwa Mbunge
wa Kuteuliwa na Rais, aliendelea na majukumu yake bungeni hadi Bunge
lilipovunjwa kupisha Uchaguzi Mkuu, ambapo alichaguliwa kuwa Mbunge na kisha Rais
Magufuli kumteua tena kuwa Waziri wa Wizara hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais Magufuli
alisema uamuzi huo ulitokana na mapendekezo ya Kamati hiyo baada ya kubaini upotevu
wa Sh trilioni 1.439, bila hatua yoyote kuchukuliwa na ofisi hizo.
Alisema anamsimamisha Mkurugenzi Mtendaji
wa TMAA kwani kwa kiasi kikubwa, amehusika na suala hilo na kuagiza achunguzwe
pamoja na wafanyakazi wengine wa Wakala huo.
“Ripoti hii haiwezi kupita hivihivi,
maana ikipita tutakuwa watu wa ajabu inabidi nifanye kitu wakati tunasubiri
ripoti nyingine, hivyo nimekubali mapendekezo ya Kamati,” alisema Rais Magufuli.
“Wizara imeshindwa kusimamia TMAA na
ujenzi wa smelter (mtambo wa kuyeyusha madini), pia haijaweka utaratibu wa
kufuatilia makanikia, walishindwa kwa nini, mbona wanasafiri kwenda Ulaya? Unashindwa
kuuliza haya makinikia yanapopakiwa hapa yanakwenda wapi upande ndege uyafuate huko!,”
alihoji Rais.
Alihoji “wakati hayo yanatokea Kamishna
wa Madini alikuwa anafanya na Waziri (Profesa Muhongo), walikuwa wanafanya
nini?
“Kwa bahati mbaya niliteua Kamishna mpya
wa madini hivi karibuni, siwezi kumhusisha kwenye hili, lakini aliyekuwapo kabla
ya huyu, zaidi ya miaka minne aangaliwe alikuwa anafanya nini,” alisema.
Alisema hawezi kuwa na watu waliosomeshwa
na nchi halafu wanafanya kazi za kipuuzi na kuvitaka vyombo vya ulinzi kuchukua
hatua kwa wahusika wa TMAA.
Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli
alisema kuanzia sasa shughuli zote za madini zitahusisha vyombo vya ulinzi na
usalama.
“Kuanzia leo vyombo vya ulinzi na
usalama vitumike vizuri maana kuna wakati eneo la kutumika polisi hawapelekwi.
Kwa nini ulinde kifaru wakati kuna eneo linalosababisha kuwepo vifaru vingi
linaachwa,” alisema.
Alibainisha kuwa katika mipaka ya nchi, watu
wanasomba madini, na kutaka uwekwe utaratibu ikiwa ni pamoja na kuorodheshwa
kwa majina, wahusika kupewa stakabadhi inayoonesha madini husika yanakopelekwa.
Alisema jambo la kushangaza ni kuwa
kampuni zinazopelekewa madini zinatajwa kwenye taarifa, lakini kuna makusudi
yalifanywa na viongozi wa sekta hiyo kwa kutonunua mtambo wa kuyeyusha madini.
“Cha ajabu, eneo ambalo yanapelekwa
madini haijapatikana, kuna tume ya nyuma ilidanganya ilikuwa inasafiri kwenda
kule na inaishia hotelini haifikishwi eneo husika,” alisema.
Taarifa
Awali akiwasilisha muhtasari wa Kamati
hiyo Mwenyekiti wake, Profesa Abdulkarim Mruma alisema Kamati ilikuwa na kazi
ya kuchunguza aina na kiwango cha madini yaliyo kwenye mchanga wa madini
unaosafirishwa nje.
Alisema chimbuko la utafiti huo ni kutokana
na kutojulikana kwa kiwango cha makinikia na mikataba yake, na kwamba kwenye
mchanga huo kumeonekana kiwango kikubwa cha madini.
Alisema hadidu za rejea zilikuwa ni kufanya
uchunguzi wa makinikia kwenye bandari ya Dar es Salaam na migodini, kufanya
uchunguzi wa kimaabara ili kujua thamani na aina ya madini yaliyo kwenye makinikia,
kuchunguza uwezo wa skena zilizo bandarini na kuchunguza uwezo wa TMAA katika
kusimamia makinikia.
Alisema Kamati ilitembelea bandari ya Dar
es Salaam, bandari kavu na migodi ya
Bulyanhulu na Buzwagi, ziliko kontena ambazo Kamati ilichukua sampuli za juu na
chini na zilizokuwa zigzaga.
Alisema pia ilichunguza uwezo wa skena
kupima makinikia na ilikokotoa thamani ya madini yaliyopatikana kwenye
makinikia.
Matokeo
Profesa Mruma alisema baada ya uchunguzi,
Kamati ilibaini uwepo wa kiasi kikubwa cha dhahabu kwenye makinikia, katika
kontena 277 zilizozuiwa ambako kulikuwa na tani saba za dhahabu.
Alisema kontena hizo 277 zilikuwa na
dhahabu yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 1.147 na kubaini uwepo wa madini
ya shaba, fedha, salfa na chuma.
Alisema shaba pekee ilikuwa na thamani
ya Sh bilioni 23.3, kukiwa na tofauti kubwa na taarifa ya Serikali iliyoonesha
kuwa na thamani ya Sh bilioni 13.
Pia, ilibaini uwepo wa fedha ya thamani
ya Sh bilioni 2.1, tofauti na taarifa ya Serikali iliyoonesha thamani ya Sh
bilioni moja.
Alisema Kamati pia ilibaini uwepo wa salfa
ya thamani ya Sh bilioni 1.9 na madini haya hayakuwa kwenye ukokotoaji wa mrabaha.
Aliongeza kuwa Kamati ilibaini uwepo wa
madini ya chuma yenye thamani ya Sh bilioni 2.3, na madini mkakati ambayo kwa
sasa yanahitajika sana duniani yakiwa na thamani ya kati ya Sh bilioni 129.5 na
Sh bilioni 261.5.
“Thamani ya madini yote katika makinikia
kwenye kontena 277 yaliyochunguzwa Kamati ilibaini kuwa na thamani ya Sh trilioni
1.339, ambazo Serikali haipati hasa senti moja na hayamo kwenye ukokotoaji wa mrabaha,”
alisema.
Profesa Mruma aliongeza kuwa Kamati iligundua
madini mengine mengi ambayo hayarekodiwi kwenye nyaraka za Serikali.
Pia, ilibaini kuwa TMAA haifungi rakili
kwenye kontena kuonesha viwango vya madini, ambapo Kamati ilibaini kuwa
ufungwaji huo hufanyika wakati wa kusafirisha kontena.
Mbali na hayo ilibaini kuwa skena za
bandarini hazina uwezo wa kubaini utoroshwaji wa madini hayo.
Mapendekezo
Kamati iliiomba Serikali kusitisha usafirishaji
wa mchanga nje ya nchi hadi mrabaha stahiki utakapolipwa kwa kuzingatia thamani
stahiki.
Aidha, iliitaka Serikali ihakikishe
mitambo ya kusafisha makinikia unajengwa nchini na TMAA ifunge rakili baada ya
mchanga kupakiwa kwenye kontena na pia ipime metal zote kwenye makininia.
Mengine ni TMAA ipime viwango vyote vya
makinikia na madini kwenye mbale bila kujali taarifa ya msafirishaji, hali
ambayo itasaidia Serikali kupata mrabaha.
Aidha, Serikali iwachukulie hatua watendaji
wa TMAA na wizara husika, na iweke mfumo wa kushitukiza kwenye udhibiti wa
madini, na itumie wataalamu wa mionzi kwenye skena za bandarini, ili kuona kama
zinaweza kufanya kazi.
Kamati hiyo ambayo iliongozwa na Profesa
Mruma iliundwa pia na Profesa Justinian Ikangula, Profesa Joseph Bushweshaiga,
Dk Yusuf Ngenya, Dk Joseph Philip, Dk Ambrose Itika, Mohamed Makongoro na Hery
Gombela.
Uundwaji wa Kamati hizo ni mkakati wa
Rais Magufuli kujiridhisha na kupata ukweli kuhusu mchanga wa madini
unasafirishwa kutoka kampuni za uchimbaji dhahabu nchini na kupelekwa nje ya
nchi kwa kinachodaiwa ni kwenda kuchenjua.
Rais Magufuli amekuwa akilalamikia
utaratibu huo wa kusafirisha mchanga wa dhahabu hata kabla ya kuwa Rais, jambo
ambalo sasa aliamua kulivalia njuga baada ya kuwa mkuu wa nchi.
0 comments:
Post a Comment