Suleiman Msuya
IGP Mangu |
WADAU wa amani nchini wametaja sababu sita
za matukio yaliyohusisha matumizi ya silaha kwa siku za karibuni kuongezeka.
Wananchi hao wanaoamini katika amani
wakiwamo wasomi, wanasiasa na mwanajeshi mstaafu, wametaja sababu hizo wakati Taifa
likishuhudia matukio yanayohusisha silaha za moto kutishia, kujeruhi hata
kupoteza maisha ya watu.
Katika matukio hayo, askari na wananchi wametishiwa
kwa silaha wakiwamo viongozi wa kisiasa, pia askari na wananchi kuuawa hasa
mkoani Pwani ambako watu wanaotuhumiwa kwa ujambazi hata askari, wamekuwa
wakitumia silaha kutishia wananchi wasio na silaha.
Miongoni mwa matukio hayo ni mauaji ya
Rufiji, Kibiti na Mkurunga mkoani Pwani na askari kumtolea silaha aliyekuwa Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye wakati akitaka kuzungumza
na waandishi wa habari, Dar es Salaam.
Wakati aliyemtishia silaha Nnauye akiwa
hajajulikana, Mei 15 tukio kama hilo lilitokea Masaki ambako polisi alifyatua
risasi angani kumtishia aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mbunge wa Mkurunga,
Adam Malima kwa kinachodaiwa ni kutotii amri ya Polisi.
Wakizungumza jana na JAMBOLEO kwa
nyakati tofauti, wadau hao walisema ni vema hali hiyo ikaangaliwa kwa jicho la
ziada, huku wakitaja sababu za matukio hayo.
Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, Dk Azaveli Lwaitama alitaja sababu ya hali hiyo kuwa ni kukosekana
kwa utawala wa sheria hali ambayo inaweza kusababisha hatari kwa nchi.
Alisema matukio ya kutumia silaha
ilianza enzi za Mwalimu Julius Nyerere lakini alikuwa akipewa nguvu ya kisheria,
kwani hakukuwa na Sheria ya Haki za Binadamu.
Lwaitama alisema wakati huu matukio hayo
yakitokea ni lazima wananchi na jamii kwa ujumla wahoji, kwa kuwa wanavunja sharia,
hivyo kuitaka Serikali na chama tawala kuondoa sheria zilizopo, ili kufanya
wanayoyataka.
“Matukio haya yamekuwa yakitokea kipindi
kirefu, ila sheria iliruhusu lakini katika Serikali ya Awamu ya Nne matukio
hayo yalirudia, kwa kutekwa na kuteswa kwa Dk Stephen Ulimboka na kuuawa kwa
mwanahabari Daud Mwangosi,” alisema.
Alisema matukio hayo yanaashiria kuwa CCM
inaanza kuona dalili za kupotea kisiasa, hivyo kujenga taswira ya kuogopwa ili
ichaguliwe tena.
Dk Lwaitama alisema utawala wa CCM
unaweza kuonekana mzuri kama sheria itafuatwa, lakini kinyume chake ni kujenga
mpasuko ndani ya Serikali.
Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala
alisema sababu kubwa ya matukio hayo, ni kukosekana kwa uchumi imara unaogusa
wananchi, hali ambayo inakosesha amani.
Alisema
asilimia kubwa ya vijana wana msongo wa mawazo, kwa kukata tamaa kutokana na
kukosa ajira, hivyo inaweza kuwasukuma kufanya matukio ambayo ni kinyume na
sheria.
“Nchi
yoyote pengo kati ya walionacho na wasionacho likiongezeka, litasababishia
wananchi msongo wa mawazo ambao ni rahisi kuzaa matukio ya uhalifu,” alisema.
Profesa
Mpangala alisema matukio ya Pwani yanahitaji uchunguzi wa kina wa Mamlaka husika ili kupata ufumbuzi, kwani
si jambo lililozoeleka na kuhoji sababu ya kuuawa raia tena viongozi.
Mwenyekiti
wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), Hashim Rungwe alisema anachokiona ni
wananchi kuuchoka uongozi na kushindwa kuvumilia uonevu na udhalilishaji.
“Lazima
tujiulize maswali mengi na si kutumia ubabe kama njia ya kutatua tatizo kwani
wananchi wamechoka, hali inayowasukuma kufanya yanayotokea, wanakosa
uvumilivu,” alisema.
Rungwe
alisema yanayotokea ni ishara mbaya kwa nchi inayodhamira kupiga hatua ya
kufikia uchumi wa kati, kwani ili kufikia hapo ni lazima wananchi washiriki kwa
moyo mmoja.
Katibu
Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Juju Danda alisema anachokiona ni mfumo wa uongozi
kushindwa kufuata misingi ya uongozi na kufikiria misingi isiyo sahihi.
“Mimi
naona mfumo hauna ajenda, hivyo kujikuta unakuja na ajenda za matukio, ambazo
hazigusi maisha ya wananchi, nadhani tunapaswa kuendesha nchi kwa ajenda
rasmi,” alisema.
Danda
alisema hali ya kufikia hata viongozi kutishiwa silaha wakiwa bila silaha, si
ishara nzuri na kuwa siku ikitokea wasioridhika kuwa wengi, hali itakuwa mbaya
zaidi.
Akizungumza
hali hiyo, askari mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Katibu wa
CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kapteni Mohamed Ligora, alisema kinachoondelea
sasa si utamaduni wa Tanzania, hivyo kupaswa kujitathmini upya.
Ligora
alisema kimsingi yanayotokea yanaweza kuwa na msukumo kutoka nje, hivyo
kuwataka Watanzania kutoupa nafasi msukumo huo.
“Nadiriki
kusema haya yanayotokea sasa si utamaduni wetu na haikubaliki ila naona kama
vile kuna msukumo wa nje wa maadui ambao hawapendi jitihada za Rais John
Magufuli ambaye ameonesha nia ya kuipeleka nchi katika uchumi wa kati,”
alisema.
0 comments:
Post a Comment