Mwandishi Wetu
BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imetoa
gawiwo la Sh. bilioni 1.7 kwa Serikali ambayo inamiliki asilimia 30 ya hisa zake.
Hundi ya kiasi hicho cha fedha alikabidhiwa
kwa Waziri wa Fedha na Mipango Dk.
Philip Mpango kwa niaba ya Waziri Mkuu katika hafla ya kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa
benki hiyo.
Hafla hiyo ya makabidhiano imefanyika
katika Hoteli ya Morena Mjini Dodoma ambako imebainishwa kuwa ni mara ya kwanza
kwa benki hiyo kutoa gawiwo.
Dk Mpango aliishukuru benki hiyo kwa
kuanza kutoa gawiwo kwa wanahisa wake baada ya ukame wa muda mrefu na kuelezea
matumaini yake kwamba kiasi cha gawiwo kitaongezeka zaidi miaka ijayo.
Hata hivyo, alizitaka benki zote nchini
kupunguza riba za mikopo inazotoza kwa wateja wao hasa baada ya Benki Kuu ya
Tanzania-BOT kupunguza riba za mikopo kwa mabenki kutoka asilimia 16 hadi
asilimia 12.
“Hii itakuwa mara ya kwanza kwa benki
hiyo kutoa gawiwo kwa wanahisa wake katika kipindi cha miaka 9 baada ya kuanza kupata
faida ya uwekezaji wake hapa nchini,” alisema.
Alizitaka pia taasisi za fedha nchini,
kuwekeza fedha katika kutekeleza Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo kwa njia
ya mikopo kwa wateja wao kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vitakavyosisimua uchumi
na kukuza ajira nchini.
Mpango alipongeza juhudi zilizofanywa na
benki hiyo kufanya uwekezaji mkubwa kwenye mtandao wa malipo ya kielektroniki
ikiwa ni maagizo ya Serikali kwamba malipo yote ya Serikali yafanyike benki au
kupitia miamala ya kielektroniki
“Nimefurahi kuthibitishiwa kwamba tangu
Julai Mosi 2016 hadi kufikia Aprili 30, 2017, NBC imekusanya fedha za Serikali
na kuzituma kielektroniki katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jumla ya Sh.
billioni 991” aliongeza Dk. Mpango.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki
hiyo, Nehemiah Mchechu, alieleza mkakati wa benki hiyo ni pamoja na kutoa
mikopo ambapo kwa sasa imetoa mikopo yenye thamani ya sh. trilioni 1 na
itaendelea kusogeza huduma zake kwa wananchi na wafanyabiashara wa kati na wa
chini kabisa.
“Mwaka jana benki yetu imepata faida ya
zaidi ya sh.bilioni 13 na katika mkutano mkuu wa wanahisa tuemekubaliana kutoa
gawiwo kwa wawekezaji” aliongeza Mchechu.
Alisema NBC inamilikiwa na wabia watatu,
wakiwemo kundi la Mabenki ya Barclays (ABSA Group ltd) ya Afrika Kusini,
inayomiliki hisa nyingi zaidi, Serikali ya Tanzania yenye hisa asilimia 30 huku
Benki ya Dunia (WB), kupitia Taasisi yake ya Fedha ijulikanayo kama The
International Finance Corporation (IFC), ikiwa na hisa asilimia 15.
0 comments:
Post a Comment