Suleiman Msuya
David Kafulila |
ALIYEKUWA Mbunge wa Kigoma Kusini, David
Kafulila, amemtaka Rais John Magufuli kuchunguza baadhi ya watumishi wa Idara ya
Usalama wa Taifa (TISS) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
kwa alichodai walijenga uhusiano na baadhi ya watendaji kufanikisha wizi wa
madini.
Kafulila alisema hayo jana siku moja
baada ya Rais Magufuli kupokea taarifa ya Kamati ya Kuchunguza Mchanga wenye Madini
ya Dhahabu iliyokuwa chini ya Profesa Abdulkarim Mruma.
Kamati hiyo ilibainisha kuwa katika kontena
277 kuna tani 7.8 za dhahabu zenye thamani ya Sh bilioni 676.
“Namshauri Rais aboreshe TISS kwa kuwa
na kitengo cha ujasusi wa kiuchumi kitakachomudu kukabiliana na uharamia wa
utoroshaji utajiri wa Taifa,” alisema.
Alisema ipo haja ya kutazama upya Katiba
ili ikibainika kuwa Rais yeyote aliyepita alihusika na ufisadi afikishwe kwenye
mkondo wa sheria.
Kafulila alisema katika ofisi za
viongozi wakuu - Ikulu ndipo vinapotoka vimemo kuruhusu uharamia wa namna hiyo.
“Ni ushauri wangu kwa Rais aruhusu
mchakato wa Katiba ili pamoja na mambo mengine, tuangalie mfumo wa ofisi yake
kama moja ya vyanzo vya uozo na uharamia huu,” alisema.
Alisema kampuni hizo za kimataifa
zinaiba duniani kote ikiwamo Ulaya na Marekani, isipokuwa huku kwetu zinaiba
zaidi kutokana na sera duni, sheria dhaifu, mifumo ya usimamizi dhaifu na
udhaifu wa wanaopewa nafasi kwa ujumla.
Aidha, alisema pamoja na changamoto hizo,
bado hatua hiyo ya Rais Magufuli inapaswa kuungwa mkono na kila mzalendo huku
akisisitiza kuwa ni moja ya malalamiko ya vyama vya upinzani.
“Naipongeza
Kamati kwa kazi iliyotukuka iliyojaa majaribu ya rushwa kubwa, kwani kampuni za
madini, mafuta na gesi duniani zina sifa hiyo kama alivyopata kusisitiza Profesa
Joseph Stirglitz gwiji wa uchumi na utandawazi duniani,” alisema.
Kafulila alimshauri Rais kuchukua hatua za
kisheria za ndani, kwa kuzifikisha kampuni hizo kwenye mahakama za kimataifa kama
inavyotamkwa kwenye mikataba ili kuzidai fidia kwa miaka yote ya mikataba yao.
Hali kadhalika alipendekeza mitambo na
mali za wawekezaji zishikiliwe mpaka kesi zitapomalizika. “Na hili lisisomeke
kwamba ni kukimbiza wawekezaji bali ni kukabili uharamia wa utoroshaji
rasilimali ambao hata sheria za kimataifa zinapiga vita,” alisema.
Wakati Kafulila akisema hayo, Mbunge wa
Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema hotuba ya
Rais Magufuli ni ushahidi mwingine, kama bado kuna shaka, ya mamlaka ya
kisheria kwa nchi ambayo anatuingiza kama Taifa.
“Natumia marufuku yake ya kusafirisha
mchanga wenye madini nje ya nchi kama mfano,” alisema.
Alisema zaidi ya dhahabu, mgodi wa Bulyanhulu
unazalisha pia madini ya fedha, cobalt, shaba na cadmium na ni mgodi pekee
nchini wenye madini yote hayo.
Alisema madini hayo kwa mujibu wa Sheria
ya Madini na Mikataba ya Uendelezaji Madini (MDAs) waliyopewa na Rais Benjamin
Mkapa na kurudiwa na Jakaya Kikwete, ni mali ya wawekezaji.
Mgodi wa Bulyanhulu unachenjua dhahabu kwa
asilimia 70 na asilimia 30 iliyobaki inafanyikia Japan ambayo ina mtambo wa
hayo madini mengine.
“Ndiyo maana mchanga huo umekuwa
unasafirishwa kwenda Japan tangu mwakan 2001. Sasa Rais angewaelekeza
wawekezaji wajenge kwanza hicho kiwanda nchini, kabla ya kupiga marufuku usafirishaji
mchanga,” alisema.
“Kwa kuzingatia kwamba wawekezaji hawa
wanalindwa kisheria na kimkataba, Rais angejadiliana na MDAs ili kufanya mchakato
wote ndani kwa ndani,” alisema.
Lissu alisema uamuzi wa Rais unaweza
kusababisha agombane na wawekezaji na serikali zao na mabwana wakubwa wa
kifedha duniani, ambao ndio wamiliki halisi wa rasilimali hizo.
Watampeleka kwenye mahakama za kimataifa
ambazo Mkapa na Kikwete walizikubali kuwa ndizo za migogoro kati yetu na
tuliowapa rasilimali zetu.
“Tukipelekwa huko hatuponi, kwa sababu
tutakuwa tumevunja mikataba na sheria zinazolinda wawekezaji na hatapata
anachokifikiria,” alisema.
Mwanasheria huyo alisema Rais wa
Bolivia, Evo Morales alikuta nchi ikiwa na mikataba kama hiyo alipochaguliwa
Desemba 2006, cha kwanza alichofanya ni kuiondoa nchi hiyo kwenye makubaliano
ya MIGA na kwenye Mikataba ya Uwekezaji (BITs) zilizokuwa zinalazimisha Mahakama
ya Kimataifa kwenye migogoro ya uwezekaji.
Kwa upande wake, Venant Rugabela alisema:
“Ripoti ni ripoti, uhakika wake ni uhakika wake na utekelezaji ni utekelezaji.”
Lakini hoja inarejea kuwa “ni kwa nini wahusika ambao ni wazalishaji
hawakuunganishwa katika kamati?”
Mariam Chimile alisema kilichotokea
katika taarifa, ni kuonesha dhahiri kuwa nchi imekuwa ikipoteza fedha nyingi
ambazo zingepaswa kutoa huduma za kijamii.
“Tumeshuhudia hudumia za afya,
miundombinu na nyingine nyingi ambazo zingekuwa nzuri kama madini hayo
yamejulikana,” alisema.
Chimile alisema ni wakati mwafaka kwa
Serikali kuangalia upya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 ili kuondoa mkanganyiko.
Ofisa Utawala wa NCCR-Mageuzi, Florian
Mbeo alisema ripoti ni nzuri ila suala la msingi ni kutekeleza aliyoyaagiza bila
kupepesa macho.
Mbeo alisema pamoja na ripoti hiyo kuwa
nzuri, bado kuna changamoto hasa kwenye mikataba ambayo inaoneshwa kukosewa
tangu awali na sheria kuwa na ukakasi.
“Tungefurahi kama mikataba ingejulikana
kwa kila mwanajamii ili tuweze kutoa maoni, lakini mikataba ile ni siri.
Hatujui kilichomo. Wanachukua rasilimali zetu kwa makubaliano ya siri,”
alisema.
Alisema haya yote yanayoikuta Serikali lawama
zinapaswa kuelekezwa kwao, wabunge na Baraza la Mawaziri.
Aidha, inasemekana taarifa hiyo ambayo
alikabidhiwa jana kwa ilisababisha kushuka kwa hisa za kampuni ya uchimbaji
madini ya Acacia kwenye Soko la Hisa la London, Uingereza.
0 comments:
Post a Comment