Aliyenusurika asimulia wenzake 35 walivyokufa


Aeleza namna basi lilivyokuwa likiviringika huku wao wakipiga kelele kuomba msaada

Waandishi Wetu

KUFELI kwa breki la basi la shule ya msingi ya mchepuo wa Kiingereza ya Lucy Vicent na udereva usio na uzoefu, vinahofiwa kuwa sababu ya ajali ya basi hilo iliyoua wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa basi hilo.

Akizungumza jana gazeti hili, mmoja kati ya wanafunzi wasiozidi watatu walionusurika kwenye ajali hiyo, Urusula Godfrey, alisema mvua kubwa ilikuwa ikiyesha kabla ya ajali hiyo kutokea.

Kwa mujibu wa Urusula, ghafla aliona gari limeruka ambapo yeye wanafunzi wenzake wakiwemo waliokufa katika ajali hiyo, walibaini si mruko wa kawaida na mara moja walianza kupiga kelele za kuomba msaada.

Wakati wakipiga kelele hizo bila msaada, Urusula alisema alishuudia basi hilo likianza kuserereka mpaka mtoni (Mto Marera), ambako lilipinduka na kuanza kuviringika.

Baada ya hapo Urusula alisema hakutambua kilichoendelea zaidi ya kujikuta tu yupo hospitalini, alisema na kushindwa kuendelea kusimulia mkasa huo na kuanza kububujikwa na machozi kwa uchungu.

Kamanda wa Polisi

Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema ajali hiyo ya jana ilitokea saa 3: 00 asubuhi eneo la Rhotia Kata ya Rhotia baada ya basi hilo kutumbukia katika Mto Marera ambao hutiririsha maji kwa msimu.

Kwa mujibu wa Kamanda Mkumbo, wanafunzi hao walikuwa wanasafiri na basi mali ya shule hiyo kwenda shule ya msingi ya mchepuo wa Kiingereza ya Tumaini Junior, iliyopo wilayani Karatu kufanya mtihani wa ujirani mwema wa kupimana uwezo.

Alisema baada ya kufika eneo hilo, gari lilowabeba lilifeli breki na kumshinda dereva kisha kutumbukia katika Mto Marera liliviringika mara kadhaa.

"Taarifa za awali zinaonyesha gari lilifeli breki na kumshinda dereva lakini uchunguzi bado unaendelea, ili kubaini kama ni uzembe wa dereva au gari lilikuwa bovu au la," alisema Kamanda Mkumbo.

Wazazi

Wakizungumza kwa nyakati tofauti huku wakibubujikwa machozi, baadhi ya wazazi waliokuwa wakisubiri miili ya watoto wao katika hosptali ya mkoa ya Mount Meru, walidai kuwa uongozi wa shule hiyo unapenda madera wa mishahara midogo, ambao hawana uzoefu wa kutosha kwenye udereva.

"Tunaiomba Serikali itusaidie kukagua mikataba ya watumishi pamoja na veti vya udereva, kwa kuwa shule nyingi za mchepuo wa Kiingereza zimekuwa zikiajiri madereva ambao hawajabobea na ambao hawajasoma shule za udereva, wakati tunalipa ada kubwa ya shule ili watoto wapate huduma nzuri," alidai mmoja wa wazazi, ambaye

Kuwasili kwa miili, majina

Vilio na simazi vilizizima kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo ya mkoa wakati wazazi, ndugu na jamaa walipokuwa wakitambua miili ya watoto na ndugu zao.

Majina ya wanafunzi waliokutwa na janga hilo yaliyobandikwa shuleni ni pamoja na Mteage Amos, Justine Alex, Irene Kishari, Gladness Godluck, Praise Roland, Shedrack Biketh na Juniuor Mwashuya.

Wengine ni Aisha Saidi, Gema Gerald, Rebecca Daudi, Hagai Lucas, Sada Ally, Ruth Ndemna, Musa Kassim, Neema Eliwahi, Neema Martin, Greyson Massawe na Witness Ndossa.

Pia yupo Hevenight Enock, Anarld Alex, Naomi Hosea, Rukia Altani, Eliapenda Eliud, Marion Mrema, Rehema Msuya, Sabrina Said, Oumhq Rashid, Iar Tarimo na Prisa Charles

JPM

Akitoa salamu za rambirambi, Rais John Magufuli alisema ajali hiyo imezima ndoto za watoto waliokuwa wakijiandaa kutumikia Taifa na imesababisha machungu, huzuni kwa Taifa.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari, ilieleza kuwa Rais Magufuli alipokea kwa mshituko na msikitiko makubwa taarifa ya vifo hivyo vya wanafunzi hao, walimu wawili na dereva wa basi hilo.

Kutokana na ajali hiyo Rais alimtumia salamu hizo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na kuleeza masikitiko yake na namna ajali hiyo ilivyosababisha huzuni na masikitiko makubwa kwa familia za marehemu na Taifa kwa ujumla.

“Ndugu Mkuu wa Mkoa naomba unifikishie pole nyingi kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wote wa wanafunzi, walimu na dereva waliopoteza maisha, hiki ni kipindi kigumu kwetu sote na uwaambie naungana nao katika majonzi na maombi,”alisema na kuongeza;

“Muhimu kwa sasa tuombee marehemu wote wapumzishwe mahali pema, majeruhi wapone haraka na wote walioguswa na msiba huu wawe na moyo wa subira, ustahimilivu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.”

Lowassa, Chadema

Akizungumzia tukio hilo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa alisema amepokea kwa masikitiko taarifa hiyo na kwamba ni ajali mbaya inayofanya siku hii kuwa siku mbaya kwa nchi.

“Nitoe pole wote waliopatwa na maafa hayo, natoa mwito kwa Watanzania tuwe na umoja wa kusaidiana kwa jambo litakalopaswa kufanywa katika kipindi hiki kigumu,”alisema Lowassa.

Akitoa salamu za pole Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje Chadema, John Mrema alisema Taifa limepoteza watoto wake na vijana wa kesho, ambao wangelitumikia na kulitaka Jeshi la Polisi kuchunguza chanzo na kutoa majibu mapema.

Alitoa salamu za pole kwa wazazi, wanafunzi wa Shule ya Lucky Vicent, uongozi wa shule hiyo pamoja na wananchi wote wa Tanzania kwa msiba huu mkubwa na wenye kutia simanzi na huzuni kubwa.

“Chadema tutakuwa pamoja na familia za marehemu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo, tunawataka wanachama na Watanzania wote bila kujali imani zetu tuwakumbuke wafiwa katika sala dua ili Mwenyezi Mungu awatie ujasiri wafiwa katika kipindi hiki kigumu,” alisema.

Alishauri Jeshi la Polisi nchini, matokeo ya uchunguzi huo wa kina yatumike katika kuzuia ajali nyingine za aina hiyo zisitokee siku zijazo.

ACT

Kiongozi Mkuu wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema Taifa limepoteza nguvu kazi ambayo si rahisi pengo lake kuzibwa

Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa chama hicho, Abdallah Khamis ilieleza kuwa kuwa Zitto amewapa pole waalimu wa shule hiyo, wazazi wa watoto, ndugu jamaaa na marafiki waliopoteza vipenzi vyao

Zitto amewaombea majeruhi majeruhi wapone haraka ili waendelee na masomo yao mpaka wafikie malengo waliyotarajiwa.

“ACT Wazalendo tumesikitishwa na vifo hivi vya watoto wetu pamoja na walimu wao, tunawapa pole ndugu jamaa na marafiki Mwenyezi Mungu awape nguvu ya kuhimili kipinfd hiki kigumu kwao,”Zitto alisema kupitia taarifa hiyo.


Imeandikwa na Seif Mangwangi, Arusha na Celina Mathew, Dar


Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo