Joyce Kasiki, Dodoma
Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu
Kassim Majaliwa amewatahadharisha wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri
wanaopatiwa mafunzo ya uongozi kwamba wataanza kuchukuliwa hatua iwapo watakwenda
kinyume cha utendaji wa kazi.
Akifungua
programu ya mafunzo ya uongozi kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri
kutoka mikoa sita ya Dodoma, Morogoro, Singida, Kigoma, Tabora na Katavi
yanayotolewa na Taasisi ya Uongozi, Majaliwa alisema awali viongozi
hao walikuwa hawachukuliwi hatua kwa sababu walikuwa wanafanya kazi kwa kutumia
uzoefu wa mahali walipotoka kabla ya kushika nyadhifa hizo.
"Tunajua
katika utendaji wenu mlikuwa mnakabiliwa na changamoto mbalimbali za
kiutendaji, lakini kwa kipindi chote cha mwaka mmoja tulikuwa hatuchukui hatua yoyote
dhidi yenu ni kwa sababu mlikuwa hamjapatiwa mafunzo wala semina yoyote ya
masuala ya uongozi, lakini sasa baada ya mafunzo haya tutaanza kuchukua hatua
kwa yeyote atakayefanya kazi kinyume," alisema Majaliwa na kuongeza:
"Kupitia
semina hii ya kuwajengea uwezo, tunaamini mtafanya vizuri zaidi kwa
kushirikiana na wasaidizi wenu lengo kubwa likiwa ni kuleta maendeleo katika
maeneo yenu na Taifa kwa ujumla."
Majaliwa aliwataka
viongozi hao kujenga mazoea ya kusikiliza hotuba za Rais John Magufuli kwani
nyingi zimekuwa zikitoka na maagizo wanayopaswa kuyatekeleza kwenye utendaji
wao wa kazi sambamba na kufuatilia vipindi vya kitaifa.
Kuhusu mada
zitakazotolewa, Majaliwa alisema ni pamoja na utunzaji wa nyaraka za Serikali
ambapo alisema nyaraka zenye siri za Serikali zinapaswa kutunzwa kwa umakini
mkubwa huku akiwataka wakurugenzi kuwachukulia hatua wale wote watakaohusika
katika kuvujisha au kutupa ovyo nyaraka za siri za Serikali.
"Tukisema
ni nyaraka za siri tunaamanisha hizo ni siri za Serikali ambazo hazitakiwi
kuvuka kwa namna yoyote ile hususan katika kipindi hiki cha utandawazi, haitakiwi
kuonekana karatasi lenye siri za Serikali limefungiwa maandazi au bidhaa
yoyote, mkurugenzi unapaswa kuchukua hatua haraka kwa mkuu wa idara husika,"
alisema.
Alizitaja mada
nyingine kuwa ni muundo wa Serikali huku akitaka katika eneo hilo wakuu wa
wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kufanya kazi kwa ushirikiano.
Aidha Majaliwa aliwataka
wakuu wa wilaya kuusimamia vizuri ushirika na kuchukua hatua kwa wahusika
watakaobainika kufanya ubadhirifu katika vyama hivyo bila kusita.
Pia aliwataka
viongozi hao kwa umoja wao kuhakikisha wanaondoa changamoto ya migogoro ya ardhi
inayojitokeza katika maeneo mengi nchini.
Aliewaasa
kuachana na tabia za ulevi kwenye nyumba starehe na kujiheshimu zaidi kwa kuwa
wao ni kioo cha jamii.
Awali Mtendaji
Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja alisema kwa mara ya kwanza
taasisi hiyo inatoa mafunzo ya pamoja kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi huku
akisema awali walikuwa wakitoa mafunzo hayo kwa wakuu wa wilaya pekee.
Alisema kabla ya
Agosti mwaka huu wakuu wa wilaya na wakurugenzi wote nchini watakuwa wamepatiwa
mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji.
Akimkaribisha
Waziri Mkuu, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,
Selemani Jafo alisema lengo la
mafunzo hayo ni kuwapatia mbinu za uongozi viongozi hao ili wazitumie
katika maeneo yao ili kuleta tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
0 comments:
Post a Comment