Mwandishi Wetu
JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limechagua
vijana waliohitimu kidato cha sita mwaka huu kutoka shule zote Tanzania Bara
kuhudhuria mafunzo yanayotolewa na Jeshi hilo kwa mujibu wa sheria.
Aidha, limewapangia kambi watakazokwenda
kupewa mafunzo kwa miezi mitatu na kuwataka kuripoti kuanzia Mei 25 hadi 30.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na
Kurugenzi ya Habari na Uhusiano wa JKT, vijana waliochaguliwa wamepangiwa kambi
za JKT Rawamkoma, Mara; JKT Msange,Tabora; JKT Ruvu, Pwani na JKT Makutupora, Dodoma.
Zingine ni JKT Mafinga, Iringa; JKT
Mlale, Ruvuma; JKT Mgambo; JKT Maramba,Tanga; JKT Makuyuni, Arusha; JKT
Bulombora, Kigoma, JKT Kanembwa, Kigoma na JKT Mtabila, Kigoma.
Iliongeza kuwa wahitimu wenye ulemavu wa
kuonekana kwa macho wanatakiwa kuripoti kambi ya JKT Ruvu iliyo Mlandizi, Pwani
ambayo ina miundombinu ya kuhudumia watu wa jamii hiyo.
Aidha, liliwataka vijana hao kuripoti na
vifaa kama bukta za bluu nyeusi yenye mpira kiunoni na mfuko nyuma, urefu
unaoishia magotini isiyo na zipu, raba za michezo za kijani au bluu, shuka
mbili za kulalia za bluu ya bahari pia.
Vingine ni soksi ndefu za rangi nyeusi,
nguo za kuzuia baridi kwa waliopangiwa mikoa yenye baridi, suti ya michezo ya
kijani au bluu na nauli ya kwenda kambini na kurudi.
Taarifa ilisema Mkuu wa JKT
anawakaribisha vijana wote waliochaguliwa ili kujiunga na wenzao katika
kujifunza uzalendo, umoja wa kitaifa, stadi za kazi, stadi za maisha na utayari
wa kulijenga na kulitumikia Taifa.
Aidha, ilisema orodha kamili ya majina
ya vijana waliochaguliwa maeneo ya kambi za JKT walizopangiwa na vifaa
wanavyotakiwa kwenda navyo inapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni
www.jkt.go.tz.
0 comments:
Post a Comment