Sharifa Marira, Dodoma
KAMATI ya Bunge
ya Ardhi, Maliasili na Utalii, imeishauri Serikali
kufuta asasi
zote zisizo za Serikali (NGOs) zinazofanya shughuli zake kwenye Pori
Tengefu la Loliondo na kusajili chache kwa masharti na vigezo vya kulinda na kuhifadhi
rasilimali za nchi.
Hayo yalisemwa
jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Atashasta
Nditiye,
alipowasilisha maoni ya Kamati hiyo wakati wa
uwasilishwaji wa
Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Alisema kuna NGOs
zaidi ya 25 ambazo zote zimejikita katika utalii, uhifadhi na utetezi wa wananchi
katika pori hilo.
Alisema asasi
hizo nyingi zinamilikiwa na wanasiasa na kufadhiliwa
na taasisi za
kimataifa ambazo Kamati haina uhakika na lengo lao kufadhili uhifadhi kwa kuwa
ni washindani wa kibiashara ya utalii na uhifadhi.
‘’Kamati
imegundua kuwa NGOs hizi kwa kiasi kikubwa zimekuwa
zikichangia mgogoro
unaoendelea katika eneo hilo baina ya Serikali na
wananchi kwa
kuwapotosha juu ya wajibu wao kwa uhifadhi wa
Serikali yao,’’ alisema
Nditiye.
"Kuna
sintofahamu ya matumizi ya ardhi na masharti maalumu yanayotakiwa kwenye mapori
yetu hususan kwa wawekezaji na
wananchi
wanaozunguka hifadhi na mapori tengefu," alisema
Nditiye.
Alisema Kamati
hiyo imeishauri Serikali kuweka wazi masharti ya
uwekezaji na
uwindaji katika maeneo ya mapori na uhifadhi ili kuondoa migogoro inayoendelea kwenye Pori
Tengefu la Loliondo na
maeneo mengine.
Aidha,
Mwenyekiti huyo alisema katika kuiongeza mapato Serikali,
Kamati imeshauri
kuongeza juhudi na mbinu za kisasa katika kukabiliana na ujangili na biashara
haramu ya wanyamapori, kwa kutoa mafunzo ya kupambana na maharamia.
Pia kuimarisha
ulinzi na uhifadhi wa wanyamapori walio hatarini
kutoweka, wakiwamo
faru, tembo na kudhibiti usafirishaji wa pembe za ndovu kwenye bandari na
viwanja vya ndege.
Nditiye, alisema
Serikali ina wajibu wa kushirikiana na Mamlaka husika kubaini mbinu za
kupunguza vifo vya wanyamapori
wanaokufa kwa
kugongwa na magari kwenye barabara zinazopita ndani ya hifadhi.
Pia kuongeza
juhudi za kusimamia sheria na utaratibu kwa
kushughulikia
watakaokutwa na hatia ya ujangili kwa kesi zao kusikilizwa haraka na kutoa
adhabu kali.
Serikali ilitakiwa
pia kuimarisha ulinzi wa ghala la kuhifadhia nyara
za Taifa na
kuweka kamera za usalama, vifaa vya kugundua moto
na kutoa mafunzo
ya kujikinga na kupambana na moto.
Kwa upande wa
sekta ya misitu na nyuki, Serikali ilitakiwa kuimarisha
ulinzi katika
misitu ili isivamiwe na shughuli za binadamu zisizo endelevu ukiwamo uvunaji
haramu, ufugaji, uchomaji mkaa na
kilimo.
Pia kuandaa
mipango endelevu kwa ajili ya makazi ya watu hasa katika
miji mikubwa inayozunguka
hifadhi na inayokua kwa kasi.
Mwenyekiti alisema
Serikali inapaswa kuongeza rasilimaliwatu
katika Taasisi ya
Utafiti na Misitu (TAFORI) ili kuiwezesha
kuanzisha na
kusimamia majaribio ya utafiti kikamilifu.
Pia Kamati
ilishauri Serikali kuharakisha mchakato kuamua
kwa tija ili
kuokoa gharama inazoingia kumtunza Faru Fausta ambaye yuko kwenye uangalizi
maalumu kutokana na maradhi aliyonayo na umri wake.
Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni iliishauri Serikali kumaliza mgogoro wa Loliondo uliodumu
kwa miaka 30 na kugharimu maisha ya wananchi kutokana na jamii ya wafugaji wa
bonde la Loliondo.
Waziri Kivuli wa
Maliasili na Utalii, Esther Matiko alisema mgogoro
huo unachochewa
na pande tatu zinazosigana ambazo ni wawekezaji, Serikali na wananchi .
Alisema mgogoro
huo ulichochewa na kampuni ya Otterlo Business Corporation (OBC) kupewa kibali
cha uwindaji na kumilikishwa
ardhi kinyume na
sheria za wanyamapori namba 12 ya Mwaka 1974.
Matiko aliitaka
Serikali itoe majibu ya tuhuma zinazoikabili
OBC na Serikali
na kuja na kauli kuhusu mgogoro huo, kwani kila kukicha viongozi wake
wanakinzana, jambo linalofanya wananchi waendelee kupata shida.
Waziri wa
Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe aliomba Sh 148,597,946,000
aliishukuru familia yake kwa kumfariji hata
katika sakata la
Faru John akisema alikuwa katika kipindi kigumu.
0 comments:
Post a Comment