Joyce Kasiki, Dodoma
Jenista Mhagama |
WAZIRI wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista
Mhagama, amesema hajajua bajeti ya ukimbizaji Mwenge wa Uhuru kwa nchi nzima
kutokana na gharama hizo kutofautiana kwa halmashauri.
Mhagama alitoa
kauli hiyo jana akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally
Keissy aliyetaka kujua ni kiasi cha fedha zinazotumika kukimbiza Mwenge nchi
nzima kwa mwaka.
Waziri huyo
alisema bajeti ya Mwenge huandaliwa na halmashauri husika kwa lengo la
kufanikisha mbio hizo.
Katika swali la
msingi, Mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji alitaka kujua kama Mwenge
kusudio lake ni umoja, upendo na mshikamano ni sababu gani umegeuka kueneza
chuki kwa kuadabisha au kuwaweka mahabusu baadhi ya wenyeviti wa mitaa kutokana
na kushindwa kuchangisha fedha za mbio hizo.
Pia alitaka
kujua kama kuna faida kwa Watanzania kuendelea kukimbiza Mwenge huo kila mwaka
na kama kuna faida ni zipi.
Akijibu swali hilo,
Mhagama alisema faida za Mwenge kitaifa na kimataifa ni pamoja na kuendelea
kuhamasisha ari ya wananchi kujitegemea na kuwekeza katika maeneo mbalimbali.
Aidha, alisema
Mwenge ni chombo pekee cha kujenga umoja na mshikamano na kudumisha amani pale
unakopita bila kujihusisha na itikadi za kisiasa.
“Mfano mzuri ni
kutokana na takwimu ambazo zinaonesha kuwa miradi ya maendeleo iliyozinduliwa
pamoja na kuwekwa mawe ya msingi kupitia Mwenge wa Uhuru kwa mwaka juzi ni 1,342
yenye thamani ya Sh bilioni 463.5,” alisema Mhagama.
Alisema Serikali
haina mpango wa kusitisha mbio hizo kutokana na faida na mafanikio makubwa
yanayopatikana kupitia mbio hizo.
0 comments:
Post a Comment