Veronica Simba, Dodoma
Profesa Sospeter Muhongo |
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,
amekataa kusaini maombi la uhamishaji wa leseni ya uchimbaji wa kati wa madini
ya shaba namba ML 571/2017 kutoka kwa Mtanzania David Kayongoya kwenda kampuni
ya Mechanized Minerals Supreme Mining Limited inayomilikiwa na raia wa China.
Profesa Muhongo alikataa kusaini leseni hiyo ya eneo la
ukubwa wa kilometa 0.43 za mraba lililoko Fufu, Chwamwino, Dodoma, baada ya
kubaini kuwa Mtanzania anayetaka kuhamishia leseni hiyo kwa raia wa China,
hatanufaika kwa kiwango kinachoridhisha.
Akizungumza na wawekezaji wa sekta ya madini, waliofika
wizarani juzi, kusainiwa leseni zao za uwekezaji, Profesa Muhongo alisisitiza kuwa
ni lazima wawekezaji katika sekta hiyo wazingatie maslahi ya wananchi na Taifa
kwa ujumla, wakati wanapowekeza.
Waziri Muhongo alimwagiza mwekezaji huyo wa China kujadiliana
kwa mara nyingine na Mtanzania mwenye eneo ili kuhakikisha ananufaika ipasavyo
na uwekezaji huo.
“Ili niweze kusaini leseni hii, rudini mezani, mzungumze
na kukubaliana ili David aweze kunufaika. Hatuwezi kukubali kuona Watanzania
wakidhulumiwa namna hii,” alisisitiza Waziri.
Awali, ilielezwa kuwa mkataba wa mauziano ya leseni
husika unaonesha kuwa David amepokea Sh milioni 30. Waziri alipotaka kujua
endapo kuna manufaa mengine ambayo David atapata, alielezwa kuwa ataajiriwa
katika kampuni hiyo kama kibarua, ndipo Waziri akakataa kusaini leseni husika.
Ili kuhakikisha suala hilo linatekelezwa ipasavyo, Profesa
Muhongo alimwagiza Kamishna wa Madini nchini, Benjamin Mchwampaka, kujiridhisha
kwa kupokea ahadi za maandishi kutoka kwa mwekezaji yeyote anayeomba leseni,
namna ambavyo atazingatia maslahi ya nchi, kabla ya kumpatia leseni anayoomba.
Kamishna Mchwampaka, pamoja na kuahidi kuzingatia na
kutekeleza agizo la Waziri; aliwataka wawekezaji hao kuzingatia kanuni na
miongozo ya uwekezaji kama inavyobainishwa katika Sheria ya Madini ya mwaka
2010.
0 comments:
Post a Comment