Abraham Ntambara
Kamanda Simon Sirro |
JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama
Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekusanya zaidi ya Sh milioni 400
kwa siku tano, baada ya kukamata magari na pikipiki zilizofanya makosa 13,584 barabarani.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Simon Sirro, alisema kuanzia Mei 9 hadi 14, kikosi
hicho kilifanya ukamataji wa makosa mbalimbali ya barabarani na kukusanya kiasi
hicho cha fedha.
“Idadi ya magari yaliyokamatwa ni
11,174, pikipiki 643, daladala 4,902, magari mengine (binafsi na malori) 4,376
na bodaboda waliofikishwa mahakamani kwa kutovaa kofia ngumu na kupakia
mishikaki ni sita,” alisema Sirro.
Pia, Jeshi la Polisi Kanda hiyo lilitoa
taarifa za kuuawa kwa jambazi kwa kupigwa risasi Kurasini katika jengo la Makao
Makuu ya Uhamiaji ambaye alijaribu kumnyang’anya silaha askari aliyekuwa
akisindikiza gari la kampuni ya G4S lililokuwa limebeba Sh milioni 320 zilizokuwa
zikisambazwa kwenye ATM za benki ya CRDB.
Akizungumzia kuuawa kwa jambazi, alisema
tukio hilo lilitokea juzi saa 9.50 alasiri na fedha hizo zilikuwa kwenye gari namba
T 155 DGB aina ya Nissan mali ya G4S huku likisindikizwa na askari wawili wa
FFU ambao walikuwa kwenye gari namba T 997 DGQ mali ya kampuni hiyo pia.
Alieleza kuwa katika eneo hilo, kulikuwa na watu wanne kwenye pikipiki mbili
aina ya Boxer ambazo hazikusomeka namba na wakati wahudumu wa gari hilo
wakisambaza fedha kwenye ATM, ghafla mmoja kati ya watu wale aliruka na
kumvamia askari Konstebo Adam kwa lengo la kumpora silaha ili kufanikisha
uporaji.
Alibainisha, kwamba baada ya kitendo
hicho jambazi huyo aliamriwa kusimama lakini alikaidi na ndipo akapigwa risasi
iliyomjeruhi mguuni na nyingine tumboni na kuishiwa nguvu na kuwekwa chini ya
ulinzi. Majeruhi alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH).
Aidha Kamishna Sirro alisema msako
unaendelea wa kukamata watuhumiwa wengine waliokimbia na pikipiki.
Kwa upande mwingine Jeshi hilo
linashikilia watuhumiwa 120 kwa makosa mbalimbali ya kihalifu ikiwa ni pamoja
na dawa za kulevya kutokana na msako uliofanyika kuanzia Mei 9 hadi 14.
0 comments:
Post a Comment