*Ni ile iliyoanzia bungeni kwa sakata la maji
Suleiman Msuya
Charles Kitwanga |
MWAKA mmoja baada ya Rais John Magufuli
kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, mbunge
huyo wa Misungwi ameibuka na kusema anashangaa kuona Waziri wa Maji na Umwagiliaji,
Gerson Lwenge akiendelea kuwa waziri.
Aidha, amesisitiza kuwa iwapo watu wa kijiji
cha Ihelele kilichopo jimboni kwake hawatapatiwa maji katika siku za karibuni,
atawaongoza kwenda kuzima mtambo wa kupeleka maji katika maeneo mengine.
Kitwanga aliyasema hayo jana wakati
akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka Dodoma, akimjibu Lwenge
ambaye juzi wakati akijibu hoja za wabunge walizozitoa wakati wakichangia
bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2017/18, alimtaka mbunge huyo
kuhama CCM kama anaona Serikali haijafanya lolote katika wilaya ya Misungwi.
Lwenge alisema Kitwanga alikuwa Waziri
wa Mambo ya Ndani katika Baraza la Mawaziri la Kwanza la Serikali ya Awamu ya
Tano, michango yake kuhusu tatizo la maji aliitoa mithili ya mtu anayeonesha
kuwa Serikali ya CCM haijafanya chochote.
“Sasa nataka nimuulize Kitwanga kama
yupo hapa kwamba hayo ni mamneo yake au ya wananchi? Kama ni wananchi
nitamuambia nini kimefanyika Misungwi, kwani hata juzi tumetia saini mikataba
ya maji na mwenyekiti wa halmashauri aliyekuwepo kwa ajili ya kupeleka maji
kutoka Ziwa Victoria kwa zaidi ya Sh.bilioni 38,” alisema Lwenge.
Katika maelezo yake ya jana, Kitwanga
alisema waziri Lwenge alipaswa kuja na majibu ya lini maji yatapatikana Ihelele
na si kumuambia ahame chama kwani katika swali lake hakuhusisha kuhama chama.
Mbunge huyo alisema haiwezekani maji
yasipatikane katika wilaya hiyo wakati eneo hilo kuna mradi wa kupitisha maji
kwenda mkoani Tabora.
”Hivi kweli mimi naweza kuhama CCM? na
je nikihama nitaacha kudai mahitaji ya watu wa Misungwi? Nadhani hajaelewa hoja
yangu ndio maana nashangaa ni vipi hadi leo anaendelea na uwaziri,” alisema.
Alisema changamoto ya maji inayowakabili
wananchi wake haina mjadala, ni lazima ipatiwe ufumbuzi na kama waziri anaona
kuna utani watamuonesha dhamira yao ya kuzima mtambo.
Kitwanga alisema wao hawana shida na maji
hata kama yatapelekwa hadi jijini Dar es Salaam, ila lengo la wananchi hao ni
kutaka maji hayo pia yawafikie.
“Maji yanatoka kwetu lakini hatuna. Hatutaki
kuwanyima watu maji, lakini na sisi tupate na kama hilo halioni basi mawazo
yake yana matatizo na atajuta kuzaliwa,” alisema.
Aidha, alisema anasikitishwa na mitazamo
ya baadhi ya mawaziri kuona kuwa wabunge wa CCM wanaosemea jambo fulani ni
wapinzani.
Kitwanga alisema waziri anapaswa
kutambua kuwa ni jukumu la kila mbunge kufikisha kero za wananchi wake Serikalini
ili zitatuliwe na sivinginevyo.
Wakati wa kuchangia bajeti ya wizara ya
maji na umwagiliaji alisema ataandaa wananchi zaidi ya 10,000 kwenda kuzima
mtambo wa kuleta maji Shinyanga na Tabora.
Kwa upande mwingine, Kitwanga alisema
hahofii mtu yoyote ambaye anadhamira ya kugombea ubunge katika jimbo hilo na
watapambana wakati ukifika.
Akichangia katika bajeti ya maji hivi
karibuni, Kitwanga alisema atahamasisha wananchi wa Misungwi wapatao 10,000,
waende kuzima mitambo katika chanzo cha maji ili wote wakose.
Alisema shida yake si bajeti ya wizara
hiyo na hatoweka ngumu wakati wa upitishwaji wale, ila atakachokifanya ni
kuwachochea wananchi hao huku akionekana kukasirishwa zaidi baada ya Lwenge
kusema wilaya hiyo ina maji.
0 comments:
Post a Comment