Mwandishi Wetu, Moshi
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kilimanjaro, limewakatia
umeme wadaiwa sugu, likiwamo Jeshi la Polisi, wafanyabiashara, watu binafsi na
idara za maji katika wilaya za Same na Mwanga.
Tanesco kwa sasa inawadai wateja wake zaidi ya Sh bilioni
15 huku wenye madeni makubwa wakiwa ni Polisi inayodaiwa zaidi ya Sh bilioni 1.1,
Magereza Sh milini 400 na Maji Same na Mwanga Sh milioni 300.
Akizungumza jana na gazeti hili ofisini kwake, Meneja wa
Tanesco wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mahawa Mkaka, alisema shirika hilo limekuwa na operesheni
mbalimbali na kubwa ikiwa ni ya kitaifa ya kukusanya madeni na kuwakatia umeme
ambao hawajalipa.
Mkaka alisema wameendelea kufuatilia madeni hayo, ambapo Magereza
walionesha nia ya kulipa na kurudishiwa huduma ya umeme, na ifikapo kesho watatakiwa
wawe wamekamilisha mchakato wa kulipa deni lao.
Alisema Jeshi la Polisi nalo limeendelea na michakato ya kulipa
deni lao, na kwamba wakiweka mikataba vizuri na kuonesha nia ya kulipa,
watarejeshewa huduma ya umeme.
“Tanesco kwa sasa tumeendesha operesheni kama nne, na ya
kwanza ni ya kitaifa ya kukusanya madeni na kuwakatia huduma ya umeme wateja ambao
hawajalipa, mpaka sasa tumekata umeme kwa wateja mbalimbali zikiwamo taasisi za
Serikali, kwani fedha tunazodai ni zaidi ya Sh bilioni 15, na ni endelevu mpaka
wateja wote walipe malimbikizo yao ya
madeni ya ankara za umeme,” alisema Mkaka.
Aidha, Mkaka alisema Operesheni nyingine inayoendeshwa na
shirika hilo mkoani Kilimanjaro, ni ya ukaguzi wa miundombinu ya umeme, ambayo
ilitarajiwa kuanza jana kwa lengo la kumaliza tatizo la baadhi ya wananchi
kujiunganishia umeme kinyume cha sheria na tatizo la wizi na uharibifu wa
miundombinu ya umeme.
0 comments:
Post a Comment