Jemah Makamba
HUJAFA hujaumbika. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya
waumini wa Kanisa la Moravian la Kitunda, Dar es Salaam, kufutiwa dhamana na
kupelekwa mahabusu baada ya kudai Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala,
Wilberfoce Luhwago ana mkakati wa kutoa hukumu ya kifungo dhidi yao.
Kutokana na tuhuma hizo, waumini hao waliokuwa nje kwa
dhamana, waliombwa na Hakimu huyo kuthibitisha madai yao, lakini baada ya
kushindwa aliamuru wafutiwe dhamana.
Washitakiwa hao wakiongozwa na Mchungaji Joachim Mwaseba
ni Mathew Mwakiposa, Kennedy Msangarufu,
Geofrey Kibona, Boniface Mwakilasa na Martin Mwiba na walifika mahakamani hapo
wakiwa na furaha, lakini wakaondoka wakiwa vichwa chini.
Wakati kesi hiyo ikiendelea, Mwaseba alisimama na kudai
kuwa wamekuwa wakisikia maneno kuwa mwisho wa kesi hiyo watahukumiwa kifungo.
"Tumesikia haya maneno sana na tuna hofu juu ya kesi
hii kwa hiyo tunaomba tubadilishiwe Hakimu ili tuwe na amani kwani hatuna raha
tunawaza kufungwa juu ya kesi hii," alidai Mchungaji huyo.
Kwa kauli hiyo, Luhwago alisema maneno ya Mchungaji huyo
yanaweza kugeuka ‘mwiba mchungu’ iwapo atashindwa kuithibitisha Mahakama.
"Mimi natenda haki kwa kufuata sheria na ikiwa hiyo
kauli umeisikia hapa mahakamani au kwa mtumishi wa Mahakama, basi naomba umtaje
sasa hivi na aitwe hapa aje athibitishe maneno haya,” alisema Luhwago.
Baada ya kubanwa, Mwaseba alidai kuwa maneno hayo aliyasikia
kwa mshitakiwa mwenzake, Msangarufu.
Luhwago alimtaka Msangarufu aiambie Mahakama kama
alitamka maneno hayo, naye akadai kuwa hakuyasikia mahakamani, bali kanisani
mwao.
“Kwa kuwa mmesikia maneno haya mtaani na hamna uhakika
nayo, mtarudi ndani wote ili mkirejeshwa hapa muanze upya utaratibu wa maombi
ya dhamana na mngoje jalada lenu kuhamishiwa kwa Hakimu mwingine,” alisema
Luhwago.
Washitakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kufanya fujo ndani
ya Kanisa wanalosali kwamba Agosti 21 mwaka jana waliingia na kuvunja viti na
kuwafanyia fujo waumini wenzao.
0 comments:
Post a Comment