Suleiman Msuya
CHAMA kipya cha siasa cha Restoration of the Nation Party (RPN)
kilichoanzishwa na wanawake na kujinasibu ndiyo mbadala wa CCM, kimezuiwa
kuendelea na mchakato wa kusaka wanachama.
Mmoja wa waanzilishi wa chama hicho,
Atis Atto, alithibitisha chama hicho kuzuiwa kusaka wanachama na kueleza kuwa
sasa kinasubiri maelekezo zaidi kutoka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa
nchini.
“Ni kweli mchakato wa kutafuta wanachama
umesitishwa na msajili na sasa tunasubiri maelekezo zaidi.” alisema Atto.
Hata hivyo, Naibu Msajili Sistus Nyahoza
alikanusha taarifa hizo na kufafanua kuwa “Ofisi yangu inasubiri fedha ili iendeleee
na mchakato wa kuvikagua vyama,” alisema.
Chama hicho kimetoa wito maalumu kwa waliotemwa
na chama tawala, CCM kujiunga ili kuendeleza harakati za kushika dola.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
nchini imewataja waasisi wa chama hicho kuwa ni Atis Atto ambaye pia ni
mwenyekiti wa muda na mwenzake Jenista Josia.
Licha ya kuwa hakijawa na usajili wa
kudumu, RPN kinatajwa kuwa kimbilio la baadhi ya wana-CCM, CUF na Chadema
walioumizwa kwa namna mbalimbali, ikiwamo wale walioondolewa kwenye nyadhifa
zao hivi karibuni ndani ya chama tawala, wakijipanga kumkabili Rais Magufuli
mwaka 2020.
Kuanzishwa kwa chama hicho kutafanya
vyama vya siasa nchini kufikia 20 nchini, iwapo kitapata usajili wa kudumu kwa
mujibu wa Sheria ya Usajili wa Vyama vya Siasa nchini.
Taarifa ambazo gazeti hili ilizipata
zinaeleza kuwa RPN kilianzishwa ili kusubiri wanasiasa waliomizwa kutoa CCM,
Chadema na CUF katika Uchaguzi Mkuu uliopita lakini kilikwama kupata usajili wa
kudumu.
Taarifa zaidi zinapasha kuwa baadhi ya
walioshika nyadhifa ikiwamo uwaziri katika awamu zilizopita na wakongwe wa
siasa wapo nyuma ya chama hicho kipya ambacho mwenyekiti wake wa muda, nje ya
siasa anajihusisha na tiba mbadala.
Atto mwenyewe katika mahojiano na JAMBO
LEO alisema lengo la kuanzisha chama hicho ni kuonesha Watanzania kuwa wanawake
wanaweza na kuomba wapewe nafasi ya kuwatumikia wananchi.
Licha ya kauli hiyo ya Atto, taarifa zinadai
kumekuwepo na hali ya kutoridhishwa kwa baadhi ya wanasiasa katika vyama vikuu
yaani Chadema, CCM na CUF hivyo mkakati unaondelea ni kutumia chama hicho
kupambana na Serikali iliyopo madarakani.
Taarifa zaidi zinapasha kwamba chama
hicho kilipoomba usajili walihojiwa kama wamefanya hivyo kwa hiyari au
wametumwa na wanasiasa wakongwe ili kuipa shinda Serikali ya CCM na vyama
vingine vyenye nguvu.
“Mimi nakumbia chama hicho lengo lake ni
kuchukua wanachama wengi wa CCM ambao wanaonesha kutoridhishwa na mfumo wa
uongozi wa Rais John Magufuli,” kilisema chanzo chetu.
Lakini akijibu hoja hiyo Atto alisema
RPN haihusiki na wanasiasa wakongwe wala mawaziri wa Serikali zilizopita.
“Mimi na Jenista ndio waanzilishi, lengo
letu ni kusaidia wananchi wa Tanzania. Tumesukumwa kuanzisha chama tukiamini tuna
wazo jipya tunalotaka kulifikisha kwa Watanzania na vyama vilivyopo vimeonekana
vina mambo yao binafsi,” alisema Atto.
Mwenyekiti huyo alisema Katiba ya RPN imeanisha
malengo yao ambayo kwa asilimia kubwa yanagusa maslahi ya Watanzania.
“Chama hiki hakina uhusiano wowote na
viongozi wakongwe na hili swali hata msajili aliuliza, lakini ukweli sisi tupo
kama sisi,” alisema.
Alisema wanawake wamekuwa katika harakati
za kulea jamii kuanzia nyumbani hivyo wanaamini kuwa ni fursa yao kwa sasa
kupewa nafasi ya kuongoza ili kuleta mabadiliko.
Atto alisema siasa za Tanzania wanawake
wamekuwa nyuma hivyo wao wakianza maandalizi ni lazima watashiriki kufanya
siasa zenye maendeleo.
“Wanawake ni wazazi, walezi, washauri na
viongozi hivyo ni wakati muafaka kuaminika na kupewa nafasi ya kuongoza,”
alisema.
Kuhusu Serikali ya sasa alisema kwa mtazamo
wake hajaufautilia kwa karibu kwani bado ni mapema na mkakati wake ni kuangalia
njia ya kuwatetea wananchi.
Atto alisema tofauti na siasa
anajihusisha na tiba asili na tiba mbadala Kibaha Maili Moja mkoani Pwani.
Alisema chama hicho kilikuwa kipate
usajili wa kudumu mwaka 2015 lakini wakiwa katika mchakato wa kutafuta
wanachama kwenye mikoa 10, Tanzania Bara na Visiwani walipokea taarifa kutoka
kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuwataka wasubiri.
Alisema kwa sasa wanasubiri taarifa ya
msajili ili waendelee na mchakato wa kutafuta wanachama kwani aliwaambia kuwa
lipo nje ya uwezo wao.
JAMBOLEO ilimtafuta Naibu Msajili wa
Vyama vya Siasa nchini Sixtus Nyahoza ambaye alithibitisha kuanzishwa kwa chama
hicho lakini alipinga kuhusika taarifa za kuhoji kama kinahusika na wanasiasa
wakubwa kutoka CCM na Chadema.
Nyahoza alisema RNP iliwasilisha maombi
yake ya kwanza Agosti 4,2014 ambapo Mei 8, 2015 kilipata usajili wa muda katika
ofisi hiyo.
Alisema kwa sasa vipo vyama 19 vyenye
usajili wa kudumu huku akiweka bayana kuwa vyama sita vimefutiwa usajili tangu
kuanza kwa vyama vingi hapa nchini.
Naibu msajili alivitaja vyama venye
usajili wa kudumu kuwa ni CCM, Chadema, CUF, UMD, NCCR-Mageuzi, NLD, UPDP, NRA,
ADA-TADEA, TLP, UDP, Demokrasia Makini, DP, SAU, AFP, CCK, ADC, CHAUMA na
ACT-Wazalendo.
“Vilivyofutwa ni PONA, TPP, FORD,
CHAUSTA, APPT-Maendeleo na Jahazi Asilia,” alisema.
0 comments:
Post a Comment