Ibrahim Yassin na Moses Ng’wat, Kyela
KAMATI ya Siasa
ya CCM Mkoa wa Mbeya imewasimamisha na kupendekeza kuvuliwa uanachama, madiwani
wanne wa chama hicho, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela kutokana na utovu
wa nidhamu.
Taarifa za
uhakika kutoka ndani ya chama hicho zilieleza jana kuwa, uamuzi huo ulifikiwa
juzi baada ya madiwani hao kugomea kikao cha
Kamati ya
Maadili na Uongozi wa Chama Mkoa, hali iliyosababisha suala hilo kupelekwa
katika Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mbeya na kufikia uamuzi huo.
Mgogoro wa madiwani
hao na Mwenyekiti wao umefukuta kwa muda mrefu jambo lililosababisha madiwani
19 wa CCM wakishirikiana na wenzao 12 wa Chadema, kumwandikia barua Mkurugenzi
wa Halmashauri hiyo, Musa Mgata, ili kuitisha Baraza Maalumu, kwa lengo la
kumng’oa Mwenyekiti wao baada ya kukosa imani naye.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya kikao hicho kilieleza kuwa, madiwani hao wanne waliosimamishwa na Kamati hiyo ya siasa Mkoa na kupendekeza kuvuliwa uanachama ni Lameck Mwambafula (Bujonde), Fyuda Msusi (Katumba, Songwe), Emmanuel Mwandambo (Ndandalo) na Furaha Mwasongela (Mababu).
“Mgogoro huu
umesababisha shughuli zote za Halmashauri kusimama, vikao zaidi ya vitano vya Baraza
vimeitishwa na kila wakifika wanagomea, lakini posho wanasaini… na ukiangalia
wote hawa ndio vinara, ndiyo maana nafikiri wajumbe wameona waondolewe,”
kilieleza chanzo hicho.
Chanzo kingine
kilieleza kuwa, mapendekezo hayo tayari yamewasilishwa katika ngazi ya Taifa
ambapo baadaye yatafikishwa katika Kamati ya Siasa na Halmashauri Kuu ya Taifa
kwa ajili ya kuhitimisha suala hilo baada ya kupitia mapendekezo ya Kamati ya
siasa Mkoa.
Hata hivyo, viongozi
wa chama hicho ulipoulizwa juu ya taarifa hizo za kusimamishwa na kisha kupendekeza
kuvuliwa uanachama madiwani hao, hawakukubali wala kukataa na badala yake
walisema suala hilo mchakato wake bado unaendelea.
Katibu wa CCM wa
Mkoa wa Mbeya, Willson Nkambako licha ya kukiri kushughulikia suala hilo, alisema
mchakato wake haujakamilika kwa ajili ya
vyombo vya habari na umma kujua kila kitu.
“Kweli kikao
kilikuwepo na kilishughulikia masuala ya ujenzi wa chama na suala hilo la Kyela
lilikuwa linaendelea kusuluhishwa,”
alisema
Nkambako.
Hata hivyo,
Katibu huyo aliwataka waandishi wa habari kumtafuta katibu Mwenezi wa Chama
hicho ili kupata taarifa zaidi juu ya sakata hilo.
Katibu wa Itikadi
na Uenezi wa Chama Mkoa wa Mbeya, Bashiru Madodi, alisema mapendekezo yote juu
ya uamuzi wa kikao cha Kamati ya Siasa yamewasilishwa ngazi ya juu kwa ajili ya
kuhitimisha suala hilo.
Mgogoro huo
unadaiwa kuibuka baada ya kusimamishwa kwa baadhi ya watumishi wa Halmashauri
hiyo, kutokana na tuhuma za ubadhirifu katika fedha za ushuru wa zao la kakao, Sh
milioni 733.
Watendaji hao
waliosimamishwa ambao hata hivyo walisharudishwa kazini ni Mweka Hazina wa
Halmashauri hiyo, Arafa Baraza na Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi, Salome Lyimo
waliosimamishwa kupisha uchunguzi.
Mwingine
aliyesimamishwa ni Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri hiyo, Joseph Sengelema,
kwa kinachodaiwa ni kutoa taarifa za uongozi juu ya ufisadi wa fedha hizo.
Hata hivyo, hadi
sasa bado hajarudishwa kazini, licha ya tume iliyoundwa kubaini kuwa hana kosa,
kutokana na madiwani kuendelea kugomea vikao vya mabaraza, ambavyo ndivyo
vyenye mamlaka ya kumrudisha.
0 comments:
Post a Comment