*Atangaza
ajira ya watumishi 52,000 kuziba pengo la waondokao
Mwandishi Wetu
Rais John Magufuli |
RAIS John Magufuli ametangaza kuwa Serikali
yake itatoa nyongeza ya mshahara ya mwaka na kupandisha madaraja ya kazi kuanzia
Bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2017/18.
Aidha, amepiga marufuku wafanyakazi wa
Serikali kuhamishwa kituo cha kazi bila kulipwa stahiki zake, akisema lengo la
hatua hiyo ni kuepusha madai yasiyo na sababu.
Rais Magufuli alisema hayo jana kwenye
sherehe za Sikukuu ya Mei Mosi zilizofanyika kitaifa Moshi mkoani Kilimanjaro.
Alisema Serikali ililazimika kufanya
ukaguzi wa watumishi wake wote kabla ya kufanya uamuzi wowote kuhusu maslahi ya
wafanyakazi na kwamba baada ya kuondoa watumishi hewa na wenye vyeti vya
kughushi atakaa na Baraza la Mawaziri kufanya maboresho.
“Acheni tufagie nyumba kwanza, mlitaka
nitangaze nyongeza huku wakiwamo watumishi hewa na wasio na vyeti? … Mwaka huu
tutapandisha madaraja ya kazi na kuweka nyongeza ya mishahara kuwa sawa na
madaraja stahiki ambayo yapo kisheria,” alisema.
Rais alisema mchakato wa kusafisha
watumishi wenye upungufu na hewa ulikuwa mgumu, hivyo ni wakati mwafaka kwa
ambao wanastahiki kupata promosheni kunufaika, kwani wangefanya kabla kundi la
wafanyakazi 19,000 waliondolewa lingekuwapo.
Magufuli alisema pamoja na kuongeza
mishahara na kupandisha vyeo, Serikali inatarajia kuajiri zaidi ya wafanyakazi
52,000 ili kuziba mapengo mbalimbali katika utumishi wa umma.
“Mei Mosi si kwa ajili ya Tanzania bali
duniani kote. Ni siku ya kukumbushana na kutafakari mambo kuhusu wafanyakazi na
kutatua matatizo yanayowakabili, hivyo nimechukua changamoto zenu na ninaahidi
kuzifanyia kazi,” alisema.
Alipongeza viongozi wa Shirikisho la Wafanyakazi
Tanzania (TUCTA), kwa kutambua dhamira ya Serikali, hivyo kuwaahidi kuendelea kuwapa
ushirikiano ili kuchangia maendeleo ya Taifa.
Aidha, alisema changamoto za kisheria
zinazowakabili wafanyakazi, waziri husika atazifikisha bungeni na zikipitishwa
atasaini muda huo huo.
“Nawahakikishia kuwa tunaanza ukurasa
mpya. Ndiyo maana mnaona hii siku ni tofauti. Serikali tumeamua kuimarisha
maslahi ya wafanyakazi. Na nyie muwe tayari kuchapa kazi,” alisema.
Rais Magufuli alisema wafanyakazi ndio
injini ya maendeleo katika Taifa lolote kubwa duniani, hivyo wanapaswa kufanya
kazi kwa pamoja kwa maslahi ya nchi na wananchi.
Kuhusu fao la kazi, alisema Serikali
inalifanyia kazi na kuna mchakato unaendelea mfanyakazi anapoacha ajira kabla
ya kustaafu, alipwe sehemu ya mafao.
Akizungumzia bima, alisema Serikali
inaendelea na utaratibu wa kuanzisha fao la Bima ya Ajira na wadau wameshatoa
maoni, hivyo wakati ukifika watapewa taarifa rasmi.
Akijibu hoja ya uhuru wa wafanyakazi
kujiunga na vyama vya wafanyakazi, alisema suala hilo lilishazungumzwa mwaka
jana na lipo kwa mujibu wa sheria na hakuna mwajiri aliye juu ya sheria.
Kwa upande mwingine, Rais Magufuli
ameziagiza wizara na taasisi kuunda mabaraza ya wafanyakazi kulingana na mahitaji
na kuwa kwa sasa yapo mabaraza 478.
Aidha, alitaka waajiri kutoa mikataba ya
ajira kwani ni jambo la kisheria na si hiari.
Akijibu madai ya wafanyakazi baada ya
kuhamishwa eneo la kazi, Rais aliwataka wafanyakazi kutohama eneo bila kulipwa
stahiki zao, kwani ni kinyume na sheria.
Rais Magufuli alisema hakuna sababu ya
mfanyakazi kuhamishwa bila kulipwa, kwani kinachoendelea ni lawama kwa Serikali,
jambo ambalo hataki kulisikia tena.
Aidha, kuhusu mfumuko wa bei, Rais
alisema Serikali ipo kwenye mkakati wa kuhakikisha hali hiyo inadhibitika, huku
akibainisha kuwa mvua zinazoendelea kunyesha zitafanikisha mchakato huo.
Halikadhalika Rais alisisitiza kuwa Serikali
ina mpango wa kuboresha na kufufua viwanda hali ambayo itachangia kuongezeka
kwa ajira.
Alisema kupitia mifuko ya hifadhi ya
jamii jumla ya dola za Marekani milioni 156 zitatumika kujenga viwanda nchini.
0 comments:
Post a Comment