MANCHESTER, Uingereza
TAKRIBAN watu 22—wakiwamo watoto—wamepoteza maisha huku 59 wengine wakijeruhiwa katika shambulio la kujitoa
mhanga, lililolenga vijana waliokusanyika kwenye uwanja wa michezo wa
Manchester Arena usiku wa kuamkia jana.
Shuhuda wa shambulio hilo baya kutokea
tangu lingine la Julai 7 alisimulia alivyoona nati na bolti zilivyojeruhi
vijana waliokuwa wakiburudika baada ya bomu hilo kulipuka katika eneo la wazi,
kati ya uwanja huo na kituo cha treni cha Victoria, muda mfupi baada ya onesho
la muziki wa msanii wa kizazi kipya, Ariana Grande kumalizika.
Picha moja ya tukio hilo, ilionesha
miili ya marehemu na majeruhi kwenye eneo hilo lililofurika watu wakiondoka
baada ya onesho hilo la muziki kumalizika.
Polisi jana asubuhi walithibitisha, kwamba
mtu aliyejitoa mhanga alifia ndani ya uwanja huo baada ya bomu hilo kulipuka.
Mlipuko ulipotokea, vijana waliojawa
hofu walibanana kwenye malango ya uwanja huo unaobeba watu 21,000. Mashuhuda waliyaelezea
mauaji hayo yaliyofanya eneo hilo kuonekana kama ‘ukanda
wa vita’.
Polisi wenye silaha, kikosi cha kutegua
mabomu na magari ya dharura walifurika eneo la tukio hilo lililotokea saa 4.35
usiku.
Muda mfupi baada ya saa 7.30 usiku, kitu
kingine kama mlipuko kilionekana kwenye bustani za Kanisa Katoliki karibu na uwanja
huo wa Manchester Arena, lakini baadaye polisi walithibitisha kwamba kitu hicho
kilikuwa ni vazi la kawaida.
Maofisa wa usalama wa Marekani walisema
wenzao wa Uingereza walimtambua mwanamume ambaye wanaamini ndiye aliyejitoa
mhanga.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari
saa 9 alfajiri, Konstebo Mkuu wa Polisi wa Manchester, Ian Hopkins
alithibitisha kwamba kikosi chake kinachukulia tukio hilo kama shambulio la
kigaidi.
Saa moja baadaye, nyota huyo wa muziki
wa Marekani, Grande, ambaye alinusurika katika shambulio hilo, aliandika kwenye
ukurasa wake wa mtandao wa Twitter kwamba ‘amenyong’onyezwa’.
“Kutoka moyoni mwangu, nasikitika sana
sana. Sina cha kusema,” aliongeza mwanamuziki huyo wa kike. Meneja wake,
Scooter Braun alisema: “Tunaomboleza watoto.”
Shuhuda Evie Brewster, aliyepelekwa na
mama yake kwenye onesho hilo ikiwa ni mara yake ya kwanza maishani kuhudhuria, aliiambia
MailOnline jinsi kishindo cha mlipuko huo kilivyosikika katika eneo lote hilo
la uwanja mwishoni mwa onesho.
“Ariana Grande alikuwa ndio kwanza amemaliza
na wimbo wake wa mwisho na kushuka jukwaani ndiyo mara ukasikika milio mkubwa
wa mlipuko,” alisema.
“Ghafla kila mtu alianza kulia na
kukimbilia langoni. Tuliweza kusikia ving’ora vya Polisi na magari ya wagonjwa.
Ilitisha. Kulikuwa na maelfu ya watu wakijaribu kutoka nje kwa pamoja. Walikuwa
wakilia na kupiga kelele.
“Eneo lote liligubikwa harufu ya moshi
na moto. Mlipuko huo ulikuwa kama umetokea ndani ya jengo mahali fulani.”
Hopkins alisema jana, kwamba anaamini
mtu huyo aliamua mwenyewe kutekeleza shambulio hilo na walikuwa (polisi) wakijaribu
kubaini kama alikuwa na mtandao.
Aliongeza kuwa watoto ni “miongoni mwa
marehemu” na kusema jana asubuhi: “Hili limekuwa ni tukio la kutisha sana
tulilopata kushuhudia katika Manchester Kuu na ambalo hakuna mtu aliyekuwa
akitarajia kulishuhudia.
“Familia na vijana wengi walikuwa
wamekwenda kuburudika kwenye onesho hilo kwenye uwanja wa Manchester Arena,
lakini wamepoteza maisha yao.
“Mawazo yetu yako kwa watu 22 ambao hivi
sasa tunajua wamepoteza maisha, na watu 59 waliojeruhiwa na pia kwa wapendwa
wao.”
0 comments:
Post a Comment