Suleiman Msuya
Kamanda Nsato Mssanzya |
KAMISHNA wa Mafunzo na Operesheni wa
Jeshi la Polisi Tanzania, Nsato Mssanzya, amesema matukio ya uhalifu yanayoendelea
maeneo mbalimbali nchini, hasa Kibiti na Rufiji yasitafsiriwe kuwa Taifa
limepoteza amani.
Aidha, amesema watu wanaouawa
wasihusishwe na vyama vya siasa, kwani hakuna taarifa zinazoonesha kuuawa kutokana
na vyama vyao, kwani matukio ya uhalifu yako duniani kote.
Mssanzya aliyezungumza na gazeti hili
juzi, alisema Jeshi la Polisi limejipanga kila kona kuhakikisha amani inadumu
nchini, akieleza kwamba matukio yanayotokea si taswira sahihi ya kusema Taifa
halina amani.
“Kila siku inayopita ni vigumu kutopata
taarifa ya matukio ya uhalifu, hivyo hali hiyo isihusishwe na kukosekana kwa
amani nchini, lakini pia si vema kuhusisha matukio hayo na siasa,” alisema.
Kamishna alisema hali ya usalama ni
nzuri na hakuna mwananchi anayekosa amani.
Alisema wananchi katika maeneo
yanayotajwa kuwa na uhalifu wananchi wanajihusisha na shughuli za uzalishaji
hali aliyosema inatoa tafsiri ya uwepo wa amani.
Hata hivyo, alisema Jeshi hilo
limejipanga kupambana na uhalifu bila kuangalia siasa au vyama, kwani
wanaopoteza maisha ni raia wa Tanzania.
Alisema yanayotokea Kibiti na Rufiji ni
matukio kama mengine na kinachotakiwa ni wananchi kutoa taarifa za viashiria
vya uhalifu na matukio hayo kwa Jeshi hilo, ili liweze kuyafanyia kazi haraka.
Kamishna alisema matukio mengi yanayotokea
Kibiti na Rufiji yamekuwa yakitokea vijijini, ambako hakuna polisi tofauti na
ilivyo mijini na kwamba kinachohitajika ni taarifa za haraka.
Kamishna aliwataka wananchi kushirikiana
na Jeshi hilo kufanikisha kukamata wahusika, ili waweze kuchukuliwa hatua za
kisheria.
0 comments:
Post a Comment