Mradi wa REA III waanza


Joyce Kasiki, Dodoma

UTEKELEZAJI wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA) awamu ya tatu ulianza nchi nzima Machi, Bunge limeelezwa.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani alitoa kauli hiyo bungeni jana, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Tendega (Chadema).

Katika swali lake Tendega alihoji sababu ya Serikali kushindwa kutoa huduma ya umeme katika vijiji vinavyozunguka kituo cha Tagamenda ambacho ni kikubwa kati ya vinavyosafirisha umeme wa Gridi ya Taifa, akiisema kinapokea umeme kutoka Mtera, Kidatu na Kihansi lakini vijiji vinavyokizunguka havina nishati hiyo.

Akijibu swali hilo, Dk Kalemani alisema hatua hiyo inalenga kuongeza wigo wa usambazaji umeme kwenye vijiji, vitongoji, taasisi za umma na maeneo ya pembezoni ambayo hayajafikiwa na miundombinu ikiwa ni pamoja na visiwa.

“Vijiji vya Ikuvilo, Wangama na maeneo mengine ya kijiji cha Tegamenda vimewekwa katika utekelezaji wa REA III utakaokamilika mwaka 2020/21,” alisema.

Alibainisha kuwa kazi ya upelekaji umeme kwenye vijiji hivyo itajumuisha njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 10.5, ujenzi wa njia ya umeme wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 9.7 na ufungaji wa transfoma tatu.

Hiyo alisema ni pamoja na kuunganishia umeme wateja wa awali 300 kwa gharama ya Sh bilioni 14.45.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo