Mwandishi Wetu
JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limeionya
televisheni ya Star TV kuwa itageuka adui wa tasnia ya habari, kama itaendelea
na kusudio lake la kurusha mahojiano maalumu na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Mbali na onyo hilo, TEF pia imetangaza
kumfuatilia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kutokana na kuibuka kwa
matukio mbalimbali ya kudhalilishwa waandishi wa habari kwa amri zake.
Makamu Mwenyekiti wa TEF, Deodatus
Balile alisema hayo jana katika taarifa yake kwa umma, ambapo alirejea sababu
za kususiwa kwa habari za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema Machi, TEF ilikubaliana
kutotangaza habari za Mkuu huyo wa Mkoa, baada ya kufanya uvamizi kwenye kituo
cha televisheni cha Clouds Machi 17.
Katika uvamizi huo, Mkuu wa Mkoa
aliambatana na askari wenye bunduki, ambao ulikuwa ni mwendelezo wa matukio ya
kudhalilisha vyombo vya habari.
“Uamuzi huo ulifikiwa kwa pamoja baina
ya TEF na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na kuungwa
mkono na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (Moat) na taasisi
nyingine za kihabari nchini,” alikumbusha Balile.
Alisema Mkuu huyo wa Mkoa alionekana
kudhalilisha wanahabari, kutukana na kutoheshimu taaluma ya habari.
Alifafanua kuwa baada ya uvamizi wa
Clouds, TEF ilimpa masharti mepesi Mkuu wa Mkoa ya kuomba radhi waandishi wa
habari, kama sehemu ya uungwana wa kitanzania, ili arejeshe uhusiano na tasnia
ya habari.
Kwa kuwa hajaomba radhi, TEF ilisema
uamuzi unaotaka kufanywa na kampuni ya Sahara Communications Limited wamiliki
wa Star TV, kuhojiana na Mkuu huyo ni usaliti wa hali ya juu kwa taaluma ya
habari, kwa kuwa imekubalika kutotangaza habari zozote zinazomhusu Mkuu huyo.
“Tulisema katika tamko hilo, kuwa yeyote
atakayeshirikiana na Mkuu huyo wa Mkoa, naye tutamhesabu kama adui wa tasnia ya
habari nchini.
“Kwa mantiki hiyo, tunasema ikiwa Star
TV wameamua kushirikiana naye basi ni wazi wameamua kwa hiyari yao kujitangaza
kuwa adui wa tasnia.
“Kila Mtanzania anajua jinsi ya
kupambana na adui kwa nia ya kujilinda na tasnia haitasita kufanya hivyo,”
alisema Balile.
Kuhusu Gambo, alisema TEF inafuatilia
kwa karibu uhusiano wake na vyombo vya habari kutokana na matukio ya mara kwa
mara ya kudhalilisha wanahabari kazini kwa amri zake.
Alionya kuwa ikiwa matukio hayo yataendelea,
TEF italazimika kupitia uhusiano huo.
Alipongeza vyombo vya habari; magazeti,
redio, televisheni na mitandao ya kijamii ya ndani na nje ya nchi, kutekeleza
uamuzi wa kumfungia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa uaminifu na uadilifu wa
hali ya juu, licha ya ushawishi wa hapa na pale unaotolewa na wapambe wake.
0 comments:
Post a Comment