Suleiman Msuya
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana,
amewatoa hofu wafanyakazi wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu
Dodoma (CDA) na wananchi wa Manispaa hiyo kuhusu stahiki zao.
Amebainisha kuwa Serikali imeunda tume
ya kutekeleza maagizo ya Rais John Magufuli aliyoyatoa baada ya kuivunja Mamlaka
hiyo.
Kauli hiyo ya Rugimbana imekuja siku
moja baada ya baadhi ya wananchi wa Manispaa hiyo, kuonekana katika ofisi za
CDA wakitaka kujua hatima ya viwanja na michoro waliyoomba kwa Mamlaka hiyo.
Alisema tume hiyo itahusisha Mamlaka ya
Utumishi wa Umma, ambayo itahusika na kuhamishia watumishi kwenye sekta
mbalimbali kama ardhi, serikali za mitaa na Manispaa yenyewe.
Mkuu huyo alisema pia tume itaangalia
utaratibu wa kuhamisha nyaraka ambapo ofisi ya Waziri Mkuu imechukua jukumu kwa
kushirikisha TAMISEMI ambayo inaunda tume husika na mkoa husika kupitia Katibu
Tawala wa Mkoa.
“Kwa sasa kinachofanyika ni mamlaka
zinazohusika kutafsiri agizo la Rais kivitendo, kuhakikisha watumishi wote wanasambazwa
katika ofisi mbalimbali na pia kuhakikisha wanapata haki zao,” alisema.
Alisema hakuna sababu ya wafanyakazi
kufikiria maslahi kwa sasa, kwani ndio mchakato umeanza huku akisisitiza kuwa watumishi
wote watapata kazi kwenye sekta mbalimbali.
Kuhusu wananchi kupata hati au ramani,
alisema hakuna mwananchi aliye na hati halali ya CDA atakayepewa nyingine kwa
mfumo wa Mamlaka itakayokuwapo.
“Kamati hii inashirikisha sehemu
mbalimbali, hivyo wananchi na wafanyakazi wawe na Amani, ila sasa huduma za CDA
zimesitishwa kwa muda ili kukamilisha mchakato wa kukabidhi nyaraka husika,”
alisema.
Akizungumza baada ya utiaji saini Amri
ya Rais, Rais Magufuli alisema ameivunja CDA na kuhamishia majukumu yake kwenye
Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, ili kuondoa mkanganyiko wa utoaji huduma kwa
wananchi uliokuwa ukisababishwa na mgongano kati ya vyombo hivyo viwili na pia
kuendana na mahitaji ya sasa ambayo yamedhihirisha kuwa hakuna haja ya CDA.
Magufuli pia aliivunja Bodi ya CDA, na
kusema aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa CDA, Paskasi Muragili atapangiwa kazi
nyingine na kuagiza wafanyakazi wote wa Mamlaka hiyo wahamishiwe Halmashauri ya
Manispaa ya Dodoma na ofisi zingine za Serikali kadri inavyofaa.
Aidha, aliagiza hati zote za kumiliki
ardhi zilizokuwa zikitolewa na CDA kwa ukomo wa umiliki wa miaka 33
zibadilishwe na kufikia ukomo wa umiliki wa miaka 99 kama ilivyo katika maeneo
mengine nchini, ili kuvutia wawekezaji hasa wa viwanda.
CDA ilianzishwa kwa Amri ya Rais Aprili
mosi 1973 na kutangazwa kupitia Tangazo la Serikali namba 230 na ilivunjwa
rasmi Mei 15 kwa Amri ya Rais na kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali.
0 comments:
Post a Comment