Mwandishi Wetu
Kassim Majaliwa |
WAZIRI Mkuu,
Kassim Majaliwa, amewataka maofisa wanaosimamia sekta ya utalii nchini
kuitangaza kwa nguvu ili kuvutia watalii wengi zaidi.
Akizungumza
katika mkutano wa 10 wa Baraza la Taifa la Biashara, Ikulu jijini Dar es Salaam
hivi karibuni, Majaliwa alisema kuna fedha nyingi serikali inazikosa katika
utalii kwa kushindwa kutangaza vivutio vyake.
“Sekta binafsi
ndiyo itakayotupa mwelekeo wa uchumi wetu hatuna budi kutilia nguvu mambo
muhimu, kama kuna tatizo liletwe katika meza ya majadiliano tujue namna ya
kulitatua,” alisema.
Alisema Tanzania
bado iko nyuma kwenye utalii na maeneo mengi ya wazi hatuyatumiki kuweka
matangazo.
“Ukienda viwanja
vya michezo hakuna matangazo, barabara hizi kuanzia mwanzo hadi mwisho yamejaa
matangazo ya kampuni za simu pekee, ukishuka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
Julius Nyerere hukuti tangazo lolote la utalii. Kuanzia leo natoa agizo taasisi zote za utalii zitangaze vivutio vyake.
Mbuga zetu zina vivutio vingi vitangazeni tena mtangaze vizuri sio mnajitangaza
bila kufuata mpangilio,” alisema Majaliwa.
Awali baadhi ya
wajumbe waalikwa kwenye mkutano huo walipopata fursa ya kuzungumzia changamoto
wanazokumbana nazo kwenye sekta ya utalii walisema kikubwa ni kutoshirikishwa
kwenye uundwaji wa sera hasa suala la tozo na Kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT).
Mkurugenzi wa
Kibo Guides, kampuni inayojishughulisha na kutembeza watalii na hoteli jijini
Arusha, Willy Chambulo alisema:
“Sekta binafsi
inajitahidi kuliletea Taifa mapato lakini hatupati mrejesho mzuri.”
Akitoa ushauri
alisema: “Kuwepo mawasiliano ya mara kwa mara kati ya taasisi za Serikali na
wafanyabiashara, suala hili ni letu sote na tunafurahi tunapoiingizia mapato
Serikali yetu lakini tuelezwe hata mwaka mmoja kabla ili tujipange.”
Waziri wa
Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema ni lazima kodi ilipwe ili
kulinda mazingira katika maeneo ya utalii na wanyama kupata huduma ikiwemo
ulinzi na matibabu.
0 comments:
Post a Comment