Abraham Ntambara
JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama
Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Saalam kitawafikisha mahakamani madereva
tisa waliobainika kuendesha mabasi ya wanafunzi bila leseni stahiki.
Kamishna Msaidizi wa Trafiki wa Kanda
hiyo, Awadh Haji alisema jana kuwa tangu waanze operesheni ya kukagua ubora wa
mabasi hayo, 185 yalikaguliwa na 119 kubainika na upungufu.
“Hadi Mei 22 tulibaini madereva tisa
wakiendesha mabasi bila leseni, hivyo tutawapeleka mahakamani,” alisema
Kamishna Haji.
Alisema katika operesheni hiyo, kuna
magari yalibainika kuwa na uchakavu wa bodi, hayana mikanda, viti kulegea na
matairi mabovu na baadhi ya magari hayo kuwa na ubovu kwenye mifumo.
Aliitaja wilaya ya Kinondoni kuongoza
kwa kuwa na magari yasiyofaa kubeba wanafunzi ikifuatiwa na Ilala huku Temeke
ikiwa ya mwisho.
Kamishna Haji alisema operesheni hiyo ni
endelevu ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi.
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama
Barabarani nchini, Mohammed Mpinga alisema amewaagiza makamanda wote nchini,
kuwasilisha kwake taarifa za ukaguzi wa magari hayo haraka iwezekanavyo.
0 comments:
Post a Comment