*Serikali yang’ang’ania msamaha wa kuhukumiwa jela
*Baadhi ya washukiwa wadaiwa kuzimia, hata kupooza
Mwandishi Wetu
Angela Kairuki |
WAKATI zaidi ya watumishi 9,000 wakisimamishwa kazi
mwanzoni mwa wiki hii, baada ya kukutwa na vyeti bandia, uchunguzi wa gazeti
hili umebaini kuwa Serikali haijakubali kuwalipa mafao yao.
Taarifa za serikalini, zimesema katika mjadala wa namna
ya kumalizana na watumishi hao kibinadamu unaoendelea, Serikali imeng’ang’ania,
kuwa imewasamehe kupelekwa mahakamani.
Kwa mujibu wa sheria, watumishi hao wangepelekwa
mahakamani, wangeshitakiwa kwa kosa la jinai na adhabu yao ni pamoja na kifungo
cha miaka hadi saba jela.
Chanzo chetu cha uhakika kutoka karibu na mazungumzo
hayo, kilibainisha kuwa mjadala huo umegawanyika pande mbili, mmoja ukitaka wafanyakazi
hao wapewe mafao yao, kwa kuwa walitumia nguvu na maarifa kutumikia Serikali.
Upande huo unaosisitiza mafao yalipwe, imeelezwa kuwa umekuwa
ukidai kuwa baadhi ya waliotajwa kuwa na vyeti hivyo walishastaafu wakisubiri
mafao huku wengine wakiwa na hundi za malipo ya stahiki zao, lakini zimezuiwa
mpaka Serikali itakapotoa kibali.
Katika kujenga hoja kwa mujibu wa chanzo hicho ndani ya Serikali,
upande huo unaotaka mafao yalipwe, ulidai kuwa baadhi walikuwa kwenye likizo ya
kustaafu na wengine walishamaliza likizo, wakajaza fomu maalumu na kupewa hundi
za mafao yao, lakini mchakato umesimama.
Msimamo huo wa Serikali, umetajwa kusababisha athari za
kiafya kwa waathirika, ambao wengi wamejikuta wakipanga foleni hospitali kupata
huduma kutoka na magonjwa na ghafla wanayopata.
Pia taarifa zingine zilieleza kwamba baadhi ya
wafanyakazi wamekuwa wakizimia na
wengine kupooza kutokana na sintofahamu inayoendelea hivi sasa, kwa sababu
hakuna uhakika wa jibu la faraja kwao.
“Kwa kweli watu wanapata matatizo makubwa sana kiafya, katika
baadhi ya ofisi tunapata taarifa za wastaafu waliopooza na hii inatokana na
kwamba hawajapewa taarifa zenye matumaini,”
alieleza mtoa taarifa wetu.
Taarifa zingine kutoka ofisi kadhaa za Serikali, zinaeleza
kuwa watumishi wengi wa kada ya chini, ndio waathirika wa uhakiki huo na baadhi
wiki iliyopita, walikuwa wakijaribu kukana vyeti walivyokuwa wakitumia.
Taarifa ambazo hazikuthibitishwa kutoka Shirika la Reli
Tanzania (TRL), zilieleza kuwa mafundi wengi wa reli, wamekuwa wakidai kutopata
elimu ya sekondari, ili wachukuliwe kuwa wenye ujuzi na elimu ya msingi, lakini
kibarua kiendelee.
Wiki iliyopita, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki alisema utaratibu wa kulipa
mafao kwa watumishi hao haujakamilika.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mollel
(CCM), Angela alisema ofisi yake itaandaa utaratibu wa mafao ya wafanyakazi
hao.
Awali Amina katika swali lake, alitaka kujua hatua za
Serikali zitakazochukuliwa katika kulipa mafao ya wafanyakazi walioachishwa
kazi baada ya kukutwa na vyeti bandia.
0 comments:
Post a Comment