Richard Mwangulube, Arusha
MAENDELEO ya
elimu katika wilaya za wafugaji mkoani hapa, yamekuwa yakidhoofishwa na mila
potofu za ukeketaji watoto wa kike wakiwa shuleni na kuchangia taaluma kushuka.
Hali hiyo
imesababisha maendeleo ya taaluma kutoridhisha na kusababisha kushuka
kwa matokeo ambapo asilimia 90 ya wanafunzi wa kike wa shule za msingi na
sekondari wamebainika kukeketwa.
Utafiti
uliofanywa katika baadhi ya sekondari kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Arusha
ulionesha kuwa asilimia 90 ya wasichana kuanzia kidato cha kwanza
hadi cha sita wamekeketwa.
Hali hiyo ilielezwa
kutokana na kuendelezwa mila potofu katika maeneo hayo ambayo asilimia kubwa
ni ya wafugaji ambao wanaamini mtoto wa kike bila kukeketwa ni vigumu kupata mume.
Udhaifu wa
kamati za maendeleo za kata na za shule unatajwa pia kuendeleza mila
hiyo ya ukeketaji wasichana, jambo lililogeuka kuwa la kudumu katika jamii za
wafugaji huku wakiendesha vitendo hivyo kwa kificho.
Kwa mujibu wa utafiti
huo, katika kata ya Mwandeti, binti wa miaka 13 alikeketwa na kupoteza
maisha kwa kupoteza damu nyingi na wazazi kumzika kisiri.
Kutokana na tukio
hilo, Jeshi la Polisi lililazimika kufukua maiti kwa ajili ya uchunguzi huku wazazi wakitorokea
kusikojulikana na hawajapatikana hadi sasa.
Utafiti huo
unaonesha kuwa taarifa za baadhi ya wataalamu wa afya Mwandeti zinaonesha kuwa
asilimia 90 ya wanafunzi wa kike wamekeketwa.
Taarifa hiyo
inaonesha kwamba idadi kubwa ya watoto wa kike kupata mimba au kuolewa wakisubiri
matokeo ya kidato cha kwanza na cha pili na utoro ni baadhi ya mambo yanayoathiri
taaluma katika maeneo ya wafugaji.
Utafiti mwingine
uliofanywa katika sekondari ya Musa katika Halmashauri ya Arusha, unaonesha kuwa
hali ya ukeketaji bado ni kikwazo kwa elimu.
“Katika sekondari
za Lengijave na Oldonyosambu idadi kubwa ya wasichana wamekuwa wakiacha
masomo na kuozeshwa na wazazi wao hali ambayo imeathiri taaluma,”
alisema mwalimu ambaye hakutaka jina lake litajwe akihofia usalama wake.
0 comments:
Post a Comment