*Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa wajumuika kuaga
*Arusha
yazizima, vilio, simanzi vyatawala Samia akiongoza
Suleiman Msuya
MSIBA wa wanafunzi 33, walimu wawili na
dereva wa shule ya msingi ya Lucky Vincent ya Arusha waliokufa kwa ajali ya
basi Mei 5 Karatu, umeunganisha Watanzania ambao kwa pamoja bila kujali itikadi
zao za kisiasa jana walijumuika kutoa heshima zao za mwisho.
Wakiongozwa na Makamu wa Rais, Samia
Suluhu Hassan maelfu ya Watanzania wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa,
wazazi, ndugu, jamaa na marafiki, walishiriki tukio hilo la kuhuzunisha
lililoandika historia mpya ikizingatiwa kuwa ajali hiyo ya barabarani ni ya
kwanza kupoteza idadi kubwa ya wanafunzi kwa pamoja.
Viongozi wengine waliohudhuria kwenye
tukio hilo ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Mwenyekiti wa
ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, Mbunge wa Arusha, Godbless Lema na viongozi wa
dini.
Wengine ni Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk
Philip Mpango, Waziri wa Elimu wa Kenya, Fred Matiang'i, wabunge, wakuu wa
mikoa, wilaya na wengine wengi.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika
kwenye uwanja wa michezo Kumbukumbu ya
Shekhe Amri Abeid, Arusha, Makamu wa Rais alisema Taifa limepatwa na mshituko
mkubwa na kutaka wazazi na familia zote kuvuta subira kwani Watanzania wako
pamoja.
Alisema pamoja na dhana kuwa Mungu ndiye
mpangaji katika kila jambo, madereva wanapaswa kuwa makini katika barabara kwa
kufuata sheria za usalama barabarani.
Samia alisema watoto hao walikuwa na
ndoto nyingi na kwa familia zao, lakini kifo kimekatisha kila kitu, hivyo
kinachotakiwa ni kumwomba Mungu.
“Nafahamu walikuwa nguzo na tegemeo
kubwa kwa familia zao naomba tutumie nafasi hii kuwaombea ili wapate kuishi kwa
amani huko waendako,” alisema.
Alisema Serikali iko na wafiwa katika
kipindi hiki kigumu na kuwa tukio hilo limewafungua macho kuangalia maeneo
ambayo kwa njia moja au nyingine, yanaweza kuhusika na matukio kama hayo.
“Napenda kuwakumbusha, kuwa kila jambo
linalotupata Mungu ana nafasi yake, hivyo hatuna budi kwenda na maandiko matakatifu,
ila natoa rai kwa vyombo vyote vya usalama barabarani kuongeza umakini,”
alisema.
Alisema wanafunzi hao walikuwa katika
kutekeleza majukumu yao ya msingi ya kielimu, jambo ambalo linaongeza maumivu
zaidi kwa jamii.
Aidha, alitoa rai kwa madereva kuwa
waangalifu katika uendeshaji magari ili kupunguza ajali nchini ili kusaidia
kuokoa maisha ya Watanzania wasio na hatia.
Makamu wa Rais aliasa madereva kutotumia
kilevi zikiwamo dawa za kulevya wawapo barabarani kwani ni moja ya sababu za
ajali zinazotokea.
Makamu wa Rais aliishukuru Kenya kwa kuonesha
ushirikiano jambo alilosema linaonesha udugu wa dhati.
“Tumepata faraja kuona ndugu zetu wa
Kenya wameshiriki msiba huu, huo ndio ushirikiano wa dhati tunawashukuru sana,”
alisema.
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa
Ibrahim Juma alisema ni tukio la kuhuzunisha, kwani watoto hao walikuwa waje
kutumikia Taifa siku zijazo ila kimekuwa kinyume.
“Ulikuwepo mwanga ambao unaongoza watoto
hawa ila kilichotokea ni tofauti na matarajio yao, kinachotakiwa ni kuwaombea,”
alisema.
Akizungumzia msiba huo, Matiang'i
alisema walipokea taarifa hizo kwa mshituko mkubwa na kuwataka wafiwa kuvumilia
katika kipindi hiki kigumu.
Matiang’i alisema Rais wa Kenya, Uhuru
Kenyatta na Wakenya wote wamehuzunishwa na vifo hivyo ambavyo vimechukua nguvukazi
ya nchi.
Mbowe alisema Watanzania wanatakiwa
kuungana na kushikamana kwa pamoja ili kuwafariji wafiwa.
Alisema msiba huo umeacha pengo kubwa
kwa Taifa kutokana na ukweli kuwa vijana hao walikuwa na ndoto za kutumikia kwenye
sekta mbalimbali.
Kinana ambaye alionekana hadharani kwa
mara ya kwanza baada ya mkutano mkuu maalumu wa chama hicho, aliwaomba wafiwa
kuamini kuwa hiyo ni mipango ya Mungu na kila mmoja wao atakutana na kifo.
Profesa Ndalichako alisema sekta ya
elimu imepata pigo kubwa kwani ni dhahiri watoto hao walikuwa na ndoto za
maisha yao ya baadaye.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema kinachotakiwa ni kuombea watoto
hao ili waweze kupokewa vizuri Mbinguni.
“Msiba huu ni mgumu sana kuubeba kwa
mzazi yeyote, mimi naomba tumpe nafasi Mungu zaidi ili aweze kutenda yake,
kwani tupo ambao hatuamini kuwa ni mipango ya Mungu,” alisema.
Viongozi wa dini ambao walipata nafasi
ya kuzungumza, waliwataka wafiwa kuamini katika Mungu kwani ndiye anayejua
sababu ya vifo hivyo kwani hata wao walio hai hawajui mwisho wao ni lini.
Tukio hilo lilikutanisha maelfu ya
wakazi wa Arusha hali ambayo ilisababisha uwanja wa Shekhe Amri Abeid kufurika
watu wenye nyuso za huzuni muda wote wa kuaga.
Mapema miili ya marehemu hao ilifikishwa
uwanjani hapo kwenye majeneza yaliyobebwa na magari ya Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ).
0 comments:
Post a Comment