*CUF yake yaiangusha ya Maalim kuhusu Bodi ya Wadhamini
*Sasa
yajipanga kudai gharama za usikilizwaji wa kesi yao
Celina Mathew
Lipumba na Maalim Seif |
CUF kambi ya Profesa Ibrahim Lipumba imeibuka
kidedea mahakamani dhidi ya ile ya Maalim Seif Sharif Hamad katika kesi
iliyohusu uteuzi wa Bodi ya Wadhamini wa Chama hicho kwa kutupwa kwa ombi la
Maalim Seif na kuridhia uamuzi wa Lipumba.
Kwa uamuzi huo wa Makahama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, Dar es Salaam juzi, upande wa Lipumba umesema utadai upande wa
Maalim Seif urejeshe gharama ilizotumia wakati wa usikilizwaji wa kesi na
kwamba unaendelea na shughuli za chama.
Uamuzi huo wa Mahakama unaweza kufasiriwa
kuwa ni ushindi unaoipa nguvu kambi ya Lipumba katika uendeshaji wa CUF ambayo imekuwa
kwenye mgogoro wa uongozi, tangu Mwenyekiti huyo atangaze kurejea kwenye nafasi
yake.
Lipumba alitangaza kujiuzulu nafasi yake
muda mfupi kabla ya Uchaguzi Mkuu, mwaka juzi akidai kupinga Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) kumpitisha Edward Lowassa, kuwa mgombea urais kupitia umoja
huo akisema ni usaliti.
Hata hivyo, upande wa pili ulieleza
kushangazwa na Lipumba ukisema ni mmoja wa walioshiriki kumshawishi Lowassa
kujiunga na Ukawa ili awanie urais.
Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Abdul
Kambaya jana aliwajulisha wanachama na Watanzania kuhusu uamuzi wa Mahakama
katika kesi hiyo namba 45/2017 iliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini kutoka
upande wa Maalim Seif ukiongozwa na Joram Bashange kuwa imefutwa na Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu.
“Kesi hiyo ilifunguliwa kwenye Mahakama
ya Kisutu na upande unaomtii Maalim Seif dhidi ya upande unaosimamia Katiba ya
CUF unaoongozwa na Profesa Lipumba, ukiiomba Mahakama kutoa amri
kwa Magdalena Sakaya, Abdul Kambaya, Thomas Malima, Masoud Mhina, Zainab
Mndolwa na Salama Masoud, kutojihusisha na shughuli za chama,” alisema.
Alisema kesi hiyo ilisababisha shughuli
za chama kusimama kutokana na baadhi ya viongozi waliopachikwa, ambao si wana CUF
kufanya shughuli za chama, huku viongozi wengine wakitangazwa kusimamishwa uanachama
na timu ya Maalim Seif.
Alisema baada ya maombi hayo kutupiliwa
mbali, walalamikiwa waliruhusiwa kupeleka madai ya kufidiwa gharama za kesi.
“Kwa hiyo waheshimiwa wanachama na wananchi
kwa ujumla, tunapenda kuwajulisha kuwa kesi hiyo imekwisha na sisi viongozi
wenu tunaendelea kufanya kazi za CUF na tutachukua hatua stahiki, ikiwamo kudai
kurejeshewa gharama za chama zilizotumika wakati wa usikilizwaji wa kesi husika,”
alisema.
Uamuzi
Juzi, wakili Mashaka Ngole aliweka
pingamizi dhidi ya mashitaka hayo, akimwomba Hakimu kuyatupilia mbali.
Kwa mujibu wa Ngole, hatua hiyo
ilitokana na vifungu vya Katiba ya CUF kueleza kuwa kesi za kushitaki au
kushitakiwa hufunguliwa na Bodi ya Wadhamini ya CUF, lakini wakati kesi
ilipofunguliwa, chama hakikuwa na Bodi hiyo.
Alisema wakati kesi ilipofunguliwa,
pande zote ndio kwanza zilikuwa zimewasilisha maombi ya usajili wa Bodi mpya na
RITA haijasajili upande wowote ule kati ya pande hizo mbili.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Wilbert
Mashauri mbele ya mawakili wa pande zote mbili, wa walalamikaji, Hashim Mziray
na wa walalamikiwa Ngole, alisema ameridhika na pingamizi lililowasilishwa na walalamikiwa
dhidi ya walalamikaji.
Hakimu Mashauri alisema waliofungua kesi
hawakuwa na sifa zilizoainishwa kwenye Katiba ya CUF kama zinavyoelezwa kwenye Sheria
namba 5 inayozungumzia masuala ya uanzishwaji wa vyama vya siasa kuwa lazima
viwe na bodi iliyosajiliwa na RITA.
Alisema kwa kuwa RITA haijasajili bodi
yoyote, ni dhahiri kuwa walalamikaji hawakuwa na sifa za kisheria kufungua shauri
hilo.
Machi 19 kikao cha Baraza la Uongozi la
Taifa la CUF upande wa Maalim Seif kilichofanyika Zanzibar, kilipitisha majina
ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini na kuyapeleka RITA.
Baada ya kupeleka majina hayo, walipata taarifa
kuwa upande wa Profesa Lipumba nao ulishapeleka majina yao RITA.
Aprili 10, Maalim Seif aliituhumu ofisi
ya Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania kuwa inashinikiza RITA ipitishe majina
ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini yaliyopelekwa na upande wa Lipumba.
Maalim Seif alisema RITA ikipitisha
majina hayo, iwe tayari kubeba dhamana kwa yatakayotokea ndani ya chama.
0 comments:
Post a Comment