Mwandish Wetu
WAKANDARASI wa kampuni ya China Civil
Engeneer Construction Cooporation (CCECC), anayejenga barabara ya Mafinga hadi Nyigo
yenye kilomita 74.1 na (CRSG) anayejenga sehemu ya Nyigo hadi Igawa yenye urefu
wa kilomita 63.8, wametakiwa kuongeza kasi ya ujenzi ili barabara hizo zikamilike
kwa wakati.
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi huo,
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani amemtaka Meneja
wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Iringa Daniel Kindole kuhakikisha
ubora wake unakidhi malengo ya Serikali.
“Barabara hii ambayo ni sehemu ya
barabara kuu ya TANZAM inaunganisha bandari ya Dar es Salaam na nchi za Zambia
na Malawi, hivyo ni muhimu kwa uchumi wa nchi, sasa ni lazima isimamiwe
kikamilifu ili idumu kwa muda mrefu”, alisema.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara
hiyo, Meneja wa Tanroads, Kindole alisema tayari kilomita 18 kati ya 74.1 katika
sehemu ya kwanza ya Mafinga hadi Nyigo imeshawekwa lami na mkandarasi ameunda
timu tatu ili kuharakisha ujenzi huo.
“Ujenzi wa barabara ya Mafinga hadi Igawa
unahusisha mikoa mitatu ambapo kilomita 74.1 ziko katika mkoa wa Iringa, kilomita
52 zipo Njombe na kilomita 12 ziko Mbeya hivyo mimi pamoja na wenzangu tumejipanga
kuhakikisha barabara hii inakamilika Novemba mwakani kama ilivyopangwa”, alisisitiza.
Meneja Mradi wa ujenzi wa barabara hiyo
sehemu ya Mafinga hadi Nyigo ambayo ina kilomita 74.1 Richard Guo
amemhakikishia naibu waziri kwamba kasi yao ya ujenzi ni nzuri na barabara hiyo
imeimarishwa ili kukidhi mahitaji na itakamilika kwa wakati.
Zaidi ya sh. bilioni 116 zinatarajiwa
kutumika katika ujenzi wa barabara hiyo sehemu ya kwanza yaani Mafinga- Nyigo
kilomita 74.1 ambazo zinagharamiwa na Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia
(WB).
0 comments:
Post a Comment